Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Unywaji Maziwa yanayofanyika mkoani Katavi leo (30.05.2022), kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Mwanamvua Mrindoko na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Dkt. Batilda Buriani.

Afisa Uendeshaji wa mfuko wa uwekezaji wa UTT AMIS, Abbas Kandila (kulia) akitoa maelezo yanayohusu mfuko huo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) muda mfupi leo (30.05.2022) kabla hajafungua Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Unywaji Maziwa yanayofanyika mkoani Katavi. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Dkt. Batilda Buriani akifuatiwa na Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini, Dkt. George Msalya.
Afisa Uhusiano wa Shirika la Viwango nchini (TBS) Bi. Neema Mtemvu (kulia) akielezea huduma zinazotolewa na Shirika hilo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kushoto) muda mfupi leo (30.05.2022) kabla hajafungua Maadhimisho hayo yanayofanyika mkoani Katavi, kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko na kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Dkt. Batilda Buriani.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akipokea ufafanuzi kutoka kwa mmoja wa wafugaji (hayupo pichani) aliyefika kwenye Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Unywaji  Maziwa yanayofanyika Mkoani Katavi, Muda mfupi kabla ya kufungua Maadhimisho hayo leo (30.05.2022), Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ametoa rai kwa Watanzania kuongeza kasi ya kunywa maziwa ili kila mmoja afikie kiwango kinachoshauriwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO)  na Shirika la Chakula na Kilimo Ulimwenguni (FAO).

Mhe. Ndaki amesema hayo leo (30.05.2022) wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Unywaji Maziwa yanayofanyika kwenye Uwanja wa Azimio uliopo Mpanda mkoani Katavi.

“Binafsi sielewi kwa nini Watanzania hatunywi maziwa kwa sababu Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO) na Shirika la Chakula na Kilimo duniani (FAO), Kila Mtanzania anapaswa kutumia wastani wa lita 200 za maziwa kwa mwaka lakini mpaka sasa takwimu zinaonesha kila Mtanzania anakunywa wastani wa lita 62 tu za maziwa kwa mwaka ambazo kama tukizigawanya kwa siku 365 za mwaka mzima utaona ni kama anakunywa tone tu la maziwa kwa siku na takwimu hizo ni kwa waliohesabiwa pekee” Amesema Mhe. Ndaki.

Mhe. Ndaki ameweka wazi faida za unywaji maziwa kwa watoto hasa wanafunzi ambapo amesema kuwa kwa mujibu wa wataalam wa afya bidhaa hiyo humsaidia mtoto kuimarisha ubongo wake, kuimarisha meno, kumuongezea kumbukumbu na nguvu wakati wote, kuongeza kiwango cha madini ya wanga na madini mengine yanayohitajika mwilini na kuimairisha misuli yake.

“Maziwa ni chakula cha msingi na muhimu sana ndugu zangu Watanzania hivyo tunyweni kwa sababu yatatusaidia kwa afya zetu” Amesisitiza Ndaki.

Akielezea mikakati ya kuhakikisha kiwango cha uzalishaji wa maziwa nchini kinaongezeka, Mhe. Ndaki amesema kuwa hivi sasa Wizara yake ipo kwenye kampeni maalum ya kuelimisha na kuhamasisha ufugaji wa kisasa ambayo inalenga kuwabadilisha  wafugaji kutoka kwenye mfumo wa ufugaji wa asili unaojumuisha mifugo mingi isiyo na tija na kuwafanya kuwa na mifugo mingi yenye tija na inayoweza kubadili maisha yao.

“Kwa hivi sasa lita 1 ya maziwa ukiikuta “supermarket” inauzwa shilingi 4,000 na kwingine ni hadi 4,500 lakini kama tukiongeza kiwango cha uzalishaji wa maziwa kupitia kampeni yetu ya kuwahasisha wafugaji kufuga kisasa, bei ya hiyo lita 1 inaweza kufika hadi  shilingi 2,000 au chini ya hapo na hapo tutafanikiwa kuwafanya Watanzania wengi kumudu kununua maziwa na hivyo kuongeza kiwango cha unywaji maziwa hapa nchini” Amesema Ndaki.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Bodi ya Maziwa nchini (TDB) kwa kupeleka maadhimisho hayo mkoani humo ambapo amewataka wananchi wote wa mkoa huo kutumia fursa hiyo kujifunza namna  ya kufuga kisasa kupitia elimu mbalimbali zinazotolewa na wataalam wa sekta ya ufugaji waliopo kwenye Maadhimisho hayo.

“Lakini pia tunaamini kabisa kwamba ujio wa maadhimisho haya utaongeza mzunguko wa fedha kwa wananchi wetu, utawaongezea kipato na tunaongeza “connection” na masoko,wazalishaji na wenye viwanda ili kujifunza namna bora ya uwekezaji hivyo niombe ikiwezekana maadhimisho haya kila Mwaka yafanyike hapa Katavi na tupo tayari kwa hilo wakati wowote ule” Amesema Mhe. Mrindoko.

Mhe. Mrindoko alitumia fursa hiyo pia kuishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kusudio lake la kujenga kituo cha kukusanyia maziwa mkoani kwake ikiwa ni moja ya vituo 10 ambavyo Wizara hiyo imepanga kujenga kwa mwaka ujao wa fedha ambapo amesema kuwa kituo hicho kitaokoa kiasi kikubwa cha maziwa yaliyokuwa yakiharibika mkoani humo kutokana na kukosa miundombinu ya kuhifadhia.

“Kwetu hiyo pia ni fursa nyingine ya kuboresha soko la maziwa yanayozalishwa hapa Katavi lakini pia itatuhakikishia zaidi kuboreshwa kwa lishe ya wananchi wetu kupitia maziwa kwa sababu watakuwa na uwezo wa kupata huduma hiyo wakati wowote wakihitaji” Amesema Mhe. Mrindoko.  

 Akizungumzia mchango wa Tasnia ya Maziwa kwenye soko la ajira, Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini (TDB) Dkt. George Msalya amesema kuwa kwa mujibu wa tawimu zilizopo mpaka sasa, Lita bilioni 3.4 za maziwa ambazo huzalishwa hapa nchini zina thamani ya dola za marekani bilioni 1.2 ambazo huingia kwenye mzunguko wa wadau wote wanaojihusisha na mnyororo wa thamani wa bidhaa hiyo.

“Kwa hiyo nitoe rai kwa Watu wote kuongeza nguvu kwenye uwekezaji wa Tasnia hii kwa sababu hata kwa upande wa ajira, takwimu zinaonesha kuwa lita 1 ya maziwa hutoa ajira 4 kwa Watanzania” Amesema Dkt. Msalya.

Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Unywaji Maziwa hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha unywaji wa maziwa na kufanya tathmini ya maendeleo ya Tasnia ya Maziwa nchini.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: