WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amewataka waandishi wa habari nchini kutumia nafasi zao vizuri na kuwa kama jicho la serikali katika kutoa elimu na ufahamu kwa wananchi kuhusu sekta ya ardhi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa mkutano wa majadiliano ya wadau wa sekta ya ardhi na sekta binafsi uliofanyika jijini Dar es Salaam Mei 23, 2022.

Aidha, amewataka kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha migogoro ya ardhi inapungua kwa asilimia 100 kama siyo kutokuwepo kabisa katika jamii.

Kauli ya Waziri wa Ardhi inakuja huku kukiwa na taarifa za upotoshaji zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii hasa mtandao wa Jamii Forum kueleza kuwa migogoro ya ardhi imeanza kushamiri upya.

Dkt.Mabula alisema hayo Mei 23, 2022 wakati wa mkutano wa majadiliano ya kisekta kati ya wizara na wadau wa sekta ya ardhi uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Wadau wa sekta ya ardhi na sekta binafsi wakiwa katika mkutano wa majadiliano uliofanyiki jijini Dar es Salaam Mei 23, 2022.

‘’Ofisi zipo wazi pale mtakapotaka ufafanuzi wa sera, sheria, kanuni, na miongozo ya ardhi tushirikiane katika kutoa elimu ili kutokomeza migogoro ya ardhi’’ alisema Dkt Mabula

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, Wizara yake iko tayari muda wowote kupokea na kuchakata mapendekezo yanayoweza kuendelea kuleta mapinduzi katika sekta ya ardhi nchini.

Wizara ya Ardhi ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za utatuzi wa changamoto za sekta ya ardhi ikiwemo kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za ardhi, kuendelea kuimarisha na kuziwezesha ofisi za ardhi za mikoa katika kuhakikisha huduma zinapatikana karibu na wananchi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo Dkt Angeline Mabula akizungumza na baadhi ya wadau mara baada ya mkutano wa majadiliano wa wadau wa sekta ya ardhi na binafsi uliofanyika Mei 23, 2022. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Dkt Allan Kijazi na kulia kwa Waziri ni Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Godwill Wanga.

Aidha, katika juhudi za kurahisisha utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa wananchi, Wizara ya Ardhi imeanzisha Kituo cha Mwasiliano kwa Wateja ambapo wananchi wanaweza kuwasilisha malalamiko yao kwa njia ya simu na kutafutiwa ufumbuzi bila kufika ofisi za ardhi.

‘’Sekta ya ardhi ni moja ya nguzo muhimu ya kuwezesha kuleta maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla na utekelezaji wa majukumu ya sekta hiyo utawezesha shughuli mbalimbali za sekta nyingine na kukuza uchumi wa kipato cha kati kupitia uwekezaji katika ardhi,’alisema Dkt.Mabula.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa sekta ya ardhi wakati wa mkutano wa majadiliano ya kisekta kati ya wadau wa sekta ya ardhi na Wizara uliofanyika jijini Dar es Salaam Mei 23, 2022.

Alieleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya maboresho kwenye sekta ya ardhi kwa kutunga na kusimamia sera na sheria mbalimbali sambamba kuandaa kanuni, miongozo na kuratibu utekelezaji wa mikakati mbalimbali ndani ya sekta kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa milki salama za ardhi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii.

Pia Waziri wa Ardhi alisema sekta ya ardhi imeendelea kuwa kiungo wezeshi kwa sekta nyingine za uzalishaji zikiwemo viwanda, kilimo, mifugo miundombinu.
Share To:

Post A Comment: