Na Joachim Nyambo,Mbeya.


VIKUNDI vya wanawake na vijana vilivyofanya vizuri kwenye utekelezaji wa Mradi wa Feed The Future Tanzania Mboga na Matunda vimeahidiwa kuimarishwa zaidi ili viendelee kutoa mchango kwenye mapambano dhidi ya udumavu na utapiamlo katika mikoa ya Mbeya na Songwe.

Miongoni mwa matokeo chanya yaliyobainika katika utekelezaji wa Mradi wa Feed The Future Tanzania Mboga na Matunda ulioendeshwa kwa miaka mitano na nusu nchini katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mbeya na Songwe kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Msaada la watu wa Marekani(USAID) ni pamoja na uzalishaji wa mazao lishe yanayotumika kwa milo ya wajawazito na watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.

Lishe bora ni moja ya vipengele vitano vya Malezi Jumuishi vinavyosisitizwa katika Mpango wa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(MMMAM) ambayo kwa sasa yanasimaiwa chini ya Programu ya kitaifa ya miaka mitano ya PJT-MMMAM ya 2021/22-2025/26.

Meneja wa Mafunzo,ufuatiliaji na uthamini wa Feed The Future Tanzania Mboga na Matunda,Stephen Mruma uzalishaji wa mazao lishe kuwa sehemu ya matokeo chanya ya mradi huo katika kikao kazi cha kutoa tathmini ya mradi huo ulioanza kutekelezwa nchini tangu Januari 2017 kilichowakutanisha wadau kutoka halmashauri za mikoa ya Mbeya na Songwe kikifanyika jijini Mbeya.

Mruma alisema kwa vikundi vingi vya vijana kujihusisha na kilimo cha mbogamboga na matunda kupiatia mradi huo kuliwezesha jamii kuvipata kwa urahisi vyakula muhimu vinavyohitajika kwaajili ya lishe bora za wajawazito,mama wanaonyonyesha na pia watoto wadogo hasa iliposhauriwa na wataalamu wa afya.

Kufuatia hali hiyo wadau waliohudhuria kikao kazi hicho walisema kuna kila sababu ya vikundi vilivyofanya vizuri kwenye mradi huo kupewa msukumo zaidi wa kuendeleza uzalishaji ili kuvipa uwezo zaidi wa kuchangia kuiondoa mikoa hiyo kwenye wastani wa asilimia 43 ya udumavu unaotajwa kuwepo.

Miongoni mwa wadau walioahidi kuwa wa kwanza kuyapa uwezo makundi hayo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali,Missana Kwangura aliyesema kwakuwa mradi umekuja na majibu ya kutatua tatizo la udumavu vikundi husika vitaingizwa kwenye mpango wa Mikopo kwa vikundi vya wanawake,vijana na walemavu ambayo hutolewa kila mwaka wa fedha kutoka mapato ya ndani.

“Kumekuwa na changamoto ya udumavu na utapiamlo licha ya mikoa yetu kuongoza katika uzalishaji wa mazao mbalimbali yakiwemo ya chakula.Yote haya yamekuja kupatiwa majibu kutokana na mradi.Lazima mradi uendelezwe na vikundi vya wanawake na vijana vilivyoshirikishwa tutaviwezesha ili uzalishaji wa mazao lishe uendelezwe.” Alisema Kwangura.

Meneja miradi wa Shirika la Kilimo la wilayani Ileje mkoani Songwe(IRDO),Patrick Mwalukisa alikitaja kijiji cha Ivuna kilichopo wilayani Momba kuwa miongoni mwa maeneo yaliyokuwa na ugumu kwa kilimo cha mbogamboga na matunda kutokana na uwepo wa wafugaji korofi licha ya kuwa na mazingira rafiki ya kilimo cha bustani.

Mwalukisa alisema baada ya ujio wa Mradi wa Feed The Future Tanzania Mboga na Matunda wakazi wa kijiji hicho na maeneo ya jirani wameondokana na adha ya kufuata umbali mrefu hadi mji wa Mlowo kufuata mbogamboga na matunda na kuendesha kilimo na kudhibiti mifugo na hivyo kuwezesha jamii kupata milo bora iliyo na lishe sahihi ikiweo inayohitajikwa kwa wanawake wajawazito,wanaonyonyesha na watoto wadogo.

Alishauri serikali na wadau katika maeneo mengine kuiga mfano wa kijiji hicho namna ulivyotumia utekelezaji wa mradi husika kubadili mwenendo wa wafugaji na kutoa mwanya kwa vijana na wanawake kuendesha shughuli za kilimo cha mazao ya matunda na mbogamboga na kuanza kukiondoa kijiji kwenye mzazingira ya lishe duni,udumavu na utapiamlo.

Afisa Kilimo wilaya ya Momba,Oscar Mwilongo aliitaja kata ya Msangano wilayani hapo kuwa miongoni mwa maeneo ambayo jamii inakabiliwa na dalili za utapiamlo na udumavu kutokana na kukosa lishe bora kwa sababu ya ufinyu wa upatikanaji wa baadhi ya vyakula ikiwemo mbogamboga na matunda hatua aliyosema inasababishwa na ufugaji holela unaokwamisha kilimo cha bustani.


Akifunga Kikao kazi hicho,Katibu Tawala msaidizi mkoa wa Songwe anayesimamia Uchumi na Uzalishaji,Vansca Kulanga aliwasihi vijana na wanawake walioshiriki utekelezaji wa mradi huo kuunda vikundi ili wanufaike na mikopo kutoka kwenye halmashauri zao na kuendelea na uzalishaji.


Share To:

Post A Comment: