Wakulima zaidi ya milioni moja kunufaika na mpango wa ukopeshaji wa pembejeo sambamba na upatikanaji wa masoko ya mazao yao kupitia programu ya AFRICA-CONNECT ambayo inaratibiwa kwa pamoja na Kampuni ya Mbolea ya YARA ,Benki ya EQUITY, Wakala wa Mbegu (ASA),Kampuni ya Viuatilifu CORTEVA na Kampuni ya MURZAH WILMER RICE MILLERS.


Hayo yamesemwa jana Mei 20, 2022 Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa programu ya AFRICA-CONNECT ambapo wakulima watanufaika na mkopo wa mbegu bora,mbolea na viuatilifu pamoja na kupata huduma ya ugani na mwisho wa siku kupata soko la mazao yao.Programu hii itaanza kwa wakulima wa mpunga 100,000 kwa mwaka huu ambapo mpunga wao wote utanunuliwa na Kampuni ya Murzah Wilmar.


Akizungumza katika hafla hiyo,Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amewapongeza Kampuni ya YARA na wadau wote washirika kwa kuja na mpango wa kusaidia kukuza sekta ya kilimo nchini yenye ajenda mahsusi ya AJENDA 10/30 yenye azma ya kuikuza sekta ya kilimo kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 na kuahidi kwa niaba ya serikali kusaidia utekelezaji wa programu hii yenye lengo la kumpunguzia mzigo mkulima katika upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na kwa uhakika.


“Nawapongeza sana YARA,Equity Benki,Corteva,ASA na Kampuni ya Murzah Wilmar kwa kuja na mpango mzuri wa kumsaidia mkulima wa mpunga kuongeza uzalishaji na kumpunguzia mzigo wa pembejeo.


Hatua hii itasaidia kutoa mchango mkubwa katika kuikuza sekta ya kilimo nchini,wote ni mashahidi na mmeona dhamira njema ya Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan katika kuiendeleza na kuikuza sekta ya kilimo ambapo bajeti ya wizara ya kilimo imepanda kutoka 294bn mpaka 751bn


Serikali imejipanga kuhakikisha mkulima ananufaika na kamwe haitashirikiana na mdau au taasisi yeyote ambayo itaonesha dalili za kudhulumu au kuwanyonya wakulima. 


Kabla ya kuja kushirikiana nanyi kwenye uzinduzi wa programu hii nilitumia muda wangu kujiridhisha kama suala hili lina maslahi kwa wakulima". Alisema Mavunde. 


Aidha, Mhe. Mavunde alishauri na kuzitaka kampuni zote zinazoshirikiana kwenye programu hiyo ambayo inalenga kuwawezesha wakulima wa mpunga kuanzia uzalishaji hadi kutafuta masoko, kuongeza wigo na kuwafikia wakulima wa mazao mengine kama mahindi ili kukuza sekta ya Kilimo na kuinua uchumi wa wakulima. 


Vilevile, Mhe Mavunde alibainisha kuwa  Serikali imeweka mkazo mkubwa kwenye utafiti na uzalishaji wa mbegu bora ili nchi ijitosheleze kwa mbegu na ziada  iuzwe nje ya nchi.


Tunapaswa wadau wote kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya kilimo. Ameongeza bajeti ya umwagiliaji kutoka shilingi Bilioni 51 Mwaka 2021/2022 hadi Bilioni 366 Mwaka 2022/2023, bajeti ya mbegu imeongezeka kutoka shilingi bilioni 11 hadi bilioni 39 na bajeti ya ugani kutoka bilioni 11 hadi bilioni 15, hii haijawahi kutokea kwenye sekta ya kilimo, hakika Mhe. Rais ameweka kilimo kuwa kipaumbele chake cha kwanza" alibainisha Mhe. Mavunde.


 

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya YARA Tanzania, Bw. Winstone Odhiambo ameeleza kuwa Programu ya Africa Connect ambayo inashirikisha wadau kama ASA, Equity Bank na Kampuni ya Wilmar inalenga kuwasaidia wakulima wa mpunga kuweza kupata mikopo nafuu ya pembejeo (mbolea na mbegu) pamoja na huduma za miongozo ya uzalishaji wa mpunga na hatimaye kuwaunganisha na masoko ya uhakika na kwa kuanzia wataanza na usajili wa wakulima 100,000 wa mpunga kuelekea katika kuwafikia wakulima 1,000,000 katika mazao mbalimbali.


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Bi. Isabela Maganga amebainisha kwamba mkopo watakaotoa kwa wakulima una lengo la kumuhakikishia mkulima anapata pembejeo zote kwa wakati na mkulima atapatiwa kwanza pembejeo na kupanda mpunga wake na baadaye ndio mkopo utatoka wa kulipia pembejeo kwa wadau husika na hivyo kupunguza muda mrefu wa kulipia mkopo.Share To:

Post A Comment: