Na Catherine Mbena/SERENGETI


Wadau wa utalii wamekubaliana kufanya maboresho katika eneo la vivuko vya wanyamapori wahamao katika Mto Mara ikiwa ni maandalizi ya msimu ya utalii unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Makubaliano hayo yamefanyika katika kikao cha siku 2 kilichoketi mwishoni mwa wiki katika Hotel ya Maramara Tented iliyopo kaskazini mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Maboresho hayo ni pamoja na ujenzi wa maeneo ya kupumzikia (picnic sites) na kufanya maboresho katika eneo la kivuko namba 4 kwa kubadili sehemu ya kuangalia wanyama (observation points) ili kuwezesha watalii kuona wanyama katika kivuko namba 3 kama watabadili Sehemu ya kuvukia.

Aidha, kikao kilikubaliana kukusanya takwimu za magari ya utalii na shughuli mbalimbali zinazofanyika katika eneo hilo ili kufanya maamuzi yenye tija.

Kikao hicho ambacho kiliongozwa na Kamishna wa Uhifadhi Kanda ya Magharibi, Martin Loibooki kilihudhuriwa  na wadau mbalimbali wa utalii wakiwemo Waongoza watalii wa upande wa Kaskazini mwa Hifadhi, Kamati ya Utalii ya vivuko vya nyumbu Mto Mara, Ofisi ya Mazingira Wilaya ya Serengeti, Chuo cha Mweka, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) na vyama vya mawakala wa Utalii cha (TATO, TLTO), vyama vya waongo watalii (TTGA).


Share To:

Post A Comment: