Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto akizungumza na watendaji wa taasisi tatu za EPZA, SIDO na NDC pamoja na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) wakati wa hafla ya kukabidhi viwanda 10 vilivyobinafsishwa na kurejeshwa serikalini kwa taasisi hizo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (kushoto) akikabidhi hati ya makubaliano kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Cecilia Mwambalaswa baada ya kusaini makubaliano ya kukabidhi kiwanda kwa shirika hilo kwenye hafla ya kukabidhi viwanda 10 vilivyobinafsishwa na kurejeshwa serikalini kwa taasisi tatu iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. NDC imepewa kuendelea kiwanda cha vipuri Mang’ula.


Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (kushoto) akisaini hati ya makubaliano na Mkurugenzi wa Uwekezaji na Masoko wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Shoma Ng’wandu (kulia) kwa ajili ya kukabidhi kiwanda kwa shirika hilo kwenye hafla ya kukabidhi viwanda 10 vilivyobinafsishwa na kurejeshwa serikalini kwa taasisi tatu iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. SIDO imekabidhiwa kiwanda cha Mbeya Ceramic.


Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (kushoto) akikabidhi hati ya makubaliano kwa Mkurugenzi wa Uwekezaji na Masoko wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Shoma Ng’wandu ( kulia) kwa ajili ya kukabidhi kiwanda kwa shirika hilo kwenye hafla ya kukabidhi viwanda 10 vilivyobinafsishwa na kurejeshwa serikalini kwa taasisi tatu iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. SIDO imekabidhiwa kiwanda cha Mbeya Ceramic.


Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (kushoto) akisaini hati ya makabidhiano ya viwanda nane na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), Charles Itembe kwenye hafla ya kukabidhi viwanda 10 vilivyobinafsishwa na kurejeshwa serikalini kwa taasisi tatu iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia ni wanasheria, Martin Kolikoli wa Ofisi ya Msajili wa Hazina na Alesia Alex Mbuya kutoka EPZA.


Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (kushoto) akikabidhi hati ya makabidhiano ya viwanda nane kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), Charles Itembe kwenye hafla ya kukabidhi viwanda 10 vilivyobinafsishwa na kurejeshwa serikalini kwa taasisi tatu iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia ni wanasheria, Martin Kolikoli wa Ofisi ya Msajili wa Hazina na Alesia Alex Mbuya kutoka EPZA.

Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (kushoto) akisaini hati ya makubaliano na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko (CPB), Dk. Anselm Moshi, Shoma Ng’wandu (kulia) wakati wa hafla ya kukabidhi viwanda 10 vilivyobinafsishwa na kurejeshwa serikalini kwa taasisi za umma iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. Bodi ya Mazao Mchanganyiko imekabidhiwa kinu cha kukoboa mpunga kilichopo Kyela mkoani Mbeya na ghala la mazao wilayani Kiteto, Manyara.



(Picha zote na Ofisi ya Msajili wa Hazina)

*Ni vile vilivyorejeshwa baada ya wawekezaji `kubabaisha’

*Yaagiza kasi katika uzalishaji, ajira, kuchangia pato kwa taifa



Na Mwandishi Wetu

SERIKALI kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imekabidhi kwa taasisi nne viwanda 10 ambavyo wawekezaji wake walishindwa kuviendeleza kulingana na mikataba ya mauzo na hivyo malengo ya serikali ya kubinafsisha viwanda hivyo kutotimia.

Taasisi zilizokabidhiwa viwanda hivyo ni Mamlaka ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo (SIDO) na Bodi ya Mazao Mchanganyiko (CPB).

Agosti, mwaka jana Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, wakati huo, alitangaza na kutoa maelekezo kuhusiana na Viwanda 20 vilivyorejeshwa serikalini na kusema viwanda 10 vihamishiwe katika Taasisi za umma na Viwanda 10 vitafutiwe wawekezaji wengine kwa njia ya zabuni.

Akikabidhi viwanda hivyo jana jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto aliwapa wakuu wa taasisi hizo wiki tatu kuhakikisha kwamba wanawasilisha mpango kazi ambao utafuatiliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

"Ingawa leo nawakabidhi viwanda hivyo, mnatakiwa kuwasilisha mipango mikakati yenu ya kuendeleza viwanda hivi ifikapo Juni 20 mwaka huu,“ alisema Benedicto na kuongeza kuwa, mipango hiyo ya uwekezaji watakayowasilisha ndiyo itatumika na Ofisi ya Msajili wa Hazina kufanya zoezi la ufuatiliaji na tathmini juu ya utekelezaji wake.

Viwanda 10 ambavyo vimeelekezwa kuhamishiwa katika taasisi hizo ni TPL Shinyanga Meat Plant ambacho ni cha nyama, Mafuta Ilulu (Lindi), kiwanda cha kubangua korosho cha Nachingwea Cashewnut (Lindi), Mkata Sawmill Limited na Sikh Sawmill Limited (Tanga), National Steel Corporation cha Dar es Salaam na Mbeya Ceramic Ltd. Vingine ni Mang’ula Mechanical & Machine Tools (Morogoro), Mwanza Tanneries (Mwanza) na TPL Mbeya.

“Kati ya Viwanda hivyo, Kiwanda cha Mang’ula Mechanical & Machine Tools kitahamishiwa NDC, Kiwanda cha Mbeya Ceramic kinakwenda SIDO na Viwanda vinane vilivyobaki vinahamishiwa EPZA,” alisema Msajili wa Hazina, Benedicto.

Aliwataka viongozi wa taasisi hizo kuhakikisha kwamba wanatimiza malengo ya uwekezaji yakiwemo ya kuongeza uzalishaji, mapato kwa serikali, ajira, kuingiza teknolojia mpya katika sekta ya viwanda na uzalishaji na hatimaye kupunguza umasikini nchini.

Akifafanua zaidi alisema Kiwanda cha Mang’ula Mechanical & Machine Tools kinakabidhiwa NDC, na SIDO wamekabidhiwa Mbeya Ceramic huku viwanda saba vimekabidhiwa EPZA.

Viwanda vilivyokabidhiwa EPZA ni TPL Shinyanga Meat Plant, Mafuta Ilulu, Nachingwea Cashewnut, Mkata Sawmill Limited, Sikh Sawmill Limited, National Steel Corporation na TPL Mbeya.

Aidha Msajili Benedicto alisema Kiwanda cha Mwanza Tanneries, Msajili atakabidhi viwanja vitatu (Na. 2,4, na 5) kati ya vitano vilivyopo kwenye eneo hilo.

“Eneo lililobaki linasubiri maelekezo kutoka kwa Mamlaka kabla ya kukabidhiwa rasmi kwa kuwa kulikuwa na maelekezo mengine ambayo yalitakiwa kukamilishwa kabla ya kufanya makabidhiano rasmi na EPZA” alisema.

Kuhusu Kiwanda cha TPL Mbeya ambacho kina eneo la Kiwanda (Plot Na. 760) na eneo la malishio ya wanyama (Nsalala Ground – Plot Na. 761), Msajili alisema atakabidhi eneo la Kiwanda tu huku akiendelea kusubiri maelekezo ya Serikali kuhusu Plot Na. 761.

Aidha, kwa upande wa Kiwanda cha National Steel Corporation, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilikabidhi eneo lililopo barabara ya Saza - Chang’ombe.

Msajili pia alisema kwa upande wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko anawakabidhi kinu cha kukoboa mpunga kilichopo Wilaya ya Kyela kwa ajili ya shughuli za ukoboaji. Aidha walikabidhiwa ghala la mazao Wilaya ya Kiteto.

Awali, Mkurugenzi wa Ubinafsishaji katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mohamed Nyasama alisema taasisi hizo zimeaminiwa na Serikali, hivyo hazina budi kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza yale ambayo serikali inayatarajia katika kuimarisha uchumi wa nchi, lakini pia kusaidia ukuzaji wa ajira na kadhalika.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa taasisi zilizokabidhiwa viwanda hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa EPZA, Charles Itembe alimshukuru Msajili wa Hazina kwa kuwaamini na kuwapa jukumu la kufufua na kuendeleza viwanja ili viweze kuleta tija kwa taifa.

“Nchi inahitaji wawekezaji. Ndiyo maana hata Rais wa nchi anazunguka huku na huko kutafuta wawezekaji kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu kiuchumi. Tunajiona tuna deni kubwa kwa serikalini lakini kwa tunaamini kwa juhudi za pamoja, tutahakikisha kazi hii inafanyika na kuweza kutimiza malengo ya serikali katika uwekezaji nchini,” alisema Itembe.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko, Dk Anselm Moshi, alisema wanashukuru kwa fursa na kwamba wanakwenda kutekeleza maagizo waliyopewa huku akiahidi nchi kuwa na hifadhi ya kutosha ya chakula.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: