Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeingia makubaliano na Nchi za Kusini mwa Afrika kuunda mfuko maalum kwa kila nchi wa kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu hususan tembo.


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja(Mb) katika Kongamano la Tembo wa Afrika lililofanyika leo katika Hifadhi ya Taifa Hwange nchini Zimbabwe.


“Tumekubaliana kwamba kuwepo na mfuko maalum kwa kila nchi ambao utakuwa mahsusi kwa ajili ya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu kama tembo na pia kuwezesha wananchi wanufaike na rasilimali wanyama hao” Mhe. Masanja amefafanua.


Ameongeza kuwa mfuko huo utakapoanzishwa utawanufaisha wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi na waathirika wa wanyama hao wanaoumizwa au kuuawa kwa kuwezesha kulipwa fidia .


Mhe. Masanja amesema kuwa sambamba na hilo mkutano huo umelenga kuangalia namna jamii zinazoishi pembezoni mwa maeneo ya hifadhi kuangalia namna zinavyoweza kushirikishwa katika kutunza rasilimali za wanyama hususan tembo.


Aidha, amesema nchi hizo zimekubaliana zisiingiliwe katika maamuzi na nchi za Magharibi kwa kuwa zenyewe ndio zinahusika katika kutunza wanyama hao na pia zinazoathirika na changamoto za wanyama hao.


Kongamano hilo  limehudhuriwa na Mawaziri na Maafisa Waandamizi kutoka nchi za Botswana, Namibia, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: