Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge akiwa amempaka mtoto wakati akisubiri apatiwe chanjo Kata ya  Iguguno wilayani Mkalama wakati alipoongoza uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya polio uliofanyika Mei 18,2022. Kutoka kulia ni Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) Cuthbert Kong'ola, Dk.Ritha Willilo kutoaka Shirika la Afya Duniani (WHO) Mganga Mkuu Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick, Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Honest Nyaki, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Ibrahim Pazia na Mkuu wa wilaya hiyo, Sophia Kizigo.

Dk.Ritha Willilo kutoaka Shirika la Afya Duniani (WHO) akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ya chanjo.

Dk.Ritha Willilo kutoaka Shirika la Afya Duniani (WHO) akiwa amempakata mtoto wakati akipatiwa chanjo hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Sophia Kizigo.

Wananchi wa Iguguno wakiwa kwenye hafla hiyo ya uzinduzi wa kampeni hiyo.
 

 

Na Abby Nkungu, Singida


MKUU wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge amewaagiza Wakuu wa wilaya, Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na Manispaa mkoani humo kuhakikisha wanafikia malengo waliojiwekea kwa kuwapatia chanjo ya polio  watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano.

Akiongoza Uzinduzi wa kampeni ya siku nne ya chanjo ya matone ya polio uliofanyika  kimkoa katika Kata ya Iguguno wilayani Mkalama, Dk Mahenge alisema iwapo  malengo yatafikiwa, mkoa utakuwa na uhakika kuwa unalea Taifa ambalo litaingia kwenye shughuli za uzalishaji likiwa na afya njema. 

Aidha, aliezea kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga bajeti kubwa kwa Sekta ya afya ambapo Mkoa wa Singida ulipokea zaidi ya Sh bilioni 30 kwa mwaka huu huku hospitali za wilaya zikijengwa Ikungi, Manyoni, Mkalama na Halmashauri ya wilaya Singida pamoja na  vituo vya afya  15 katika wilaya zote.

"Nimeyasema haya ili kuonesha jinsi Rais wetu anavyotujali Watanzania na ndio maana leo tupo hapa tunazindua kampeni hii ya polio baada ya Serikali kutuwezesha" alisema Dk.Mahenge.

Awali, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Victorina Ludovick alisema kuwa mkoa  unatarajia kufikia jumla ya watoto 286,736 walio chini ya miaka mitano kwa kipindi cha siku tatu na kwamba lengo ni kufika kwenye maeneo yote ambapo itafanyika nyumba kwa nyumba .

Alitaja madhara ya ugonjwa wa Polio kuwa ni ulemavu wa ghafla wa viungo na usiotibika kwa hiyo ni muhimu kwa kila mzazi na mlezi kuwatoa watoto wao wenye umri tajwa ili wapate chanjo hiyo salama.

Dk.Ritha Willilo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) alitoa mwito kwa wazazi kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa watoa huduma ya chanjo hiyo ili malengo ya Serikali yaweze kutimia.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa waliahidi kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto wao kwenye chanjo kwa kuwa sasa wameelimika vya kutosha na kwamba wameachana na imani potofu zilizokuwa zikiwazuia kukubali chanjo mbalimbali.

Kwa mujibu wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) 2021/22 - 2025/26, Serikali ya Tanzania kupitia Sera ya Afya 2007 imewekeza sana katika kuboresha uhai wa mtoto kupitia utoaji wa huduma bure za afya kwa akinamama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: