Wahitimu wa Chuo cha Ualimu Korogwe wakiwa kwenye mahafali ya 62 ya Chuo hicho (Picha na Yusuph Mussa)

MENEJA wa Benki ya NMB Tawi la Korogwe Mwampeta Lugano  akizungumza kwenye mahafali ya 62 ya Chuo hicho (Yusuph Mussa)

MKUU wa Chuo cha Ualimu Korogwe Hassan Ismail akizungumza wakati wa maafali ya 62 ya Chuo cha Ualimu Korogwe kama mgeni rasmi(Picha na Yusuph Mussa)

Na Yusuph Mussa, Korogwe

CHUO cha Ualimu Korogwe, pamoja na kutoa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), lakini chuo hicho hakina huduma ya internet, hivyo kuwafanya wanafunzi wanaojifunza kozi hiyo kuwa ngumu wakati wa kufanya kwa vitendo.

Lakini pia, pamoja na Serikali kujenga maktaba ya kisasa kwenye chuo hicho yenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 250, lakini imeshindwa kuweka mtandao wa internet, sababu maabara hiyo pia ina  kompyuta kwa ajili ya kujisomea.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Korogwe kwenye risala iliyosomwa na Izadine Masanga kwenye mahafali ya 62 ya chuo hicho kikongwe nchini, ambapo wanachuo 724 walihitimu mafunzo ya stashahada maalumu ya ualimu ya sayansi, hisabati na TEHAMA kwa shule za sekondari.


"Pamoja na mafunzo ya TEHAMA kutolewa chuoni, maabara ya TEHAMA ni ndogo sana na haina vifaa vya kutosha kulingana na idadi ya wanachuo. Kwa mfano, upatikanaji wa vifaa kama vinukushi, printer na vingine vinavyokosekana, vinasababisha changamoto kubwa sana wakati wa kufanya mafunzo kwa vitendo (practical). Pia kukosa Mkongo wa Taifa.


"Maktaba mpya kubwa na ya kisasa kukosa mfumo wa internet pamoja na vitabu muhimu vyenye kukidhi haja katika masomo ya ngazi mbalimbali. Maombi yetu, tunaomba kuongezewa samani  hususani meza na viti kwa matumizi ya wakufunzi na wanachuo madarasani, na kuwekwa mfumo wa internet hususani maeneo ya maktaba mpya na maabara ya ICT" ilisema risala hiyo.


Mkuu wa Chuo hicho Hassan Ismail alisema moja ya changamoto chuoni hapo ni kukosa uzio, ambapo karibu eneo lote la chuo lipo wazi, na hiyo kutoa nafasi kwa wanajamii wanaokizunguka chuo kufanya njia karibu maeneo yote ya chuo  pamoja na kuchungia mifugo yao

Ismail alisema, pamoja na chuo hicho kutoa mafunzo ya sayansi, hisabati na TEHAMA, lakini maabara yake haina mtandao wa internet, huku kompyuta zilizopo kushindwa kukidhi mahitaji ya chuo hicho ambacho kinachukua wanachuo 1,200 kwa wakati mmoja, ambapo kwa sasa wapo wanachuo 1,051.


Alisema changamoto nyingine ni upungufu wa samani katika ofisi za wakufunzi na madarasani, upungufu wa vitabu vya masomo ya sayansi, hisabati na TEHAMA katika maktaba ya chuo, na uchakavu wa nyumba  za watumishi.


Mgeni rasmi kwenye mahafali hayo, Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Korogwe Lugano Mwampeta alisema katika kupunguza changamoto ya chuo hicho, benki ya NMB itatoa viti na meza vyenye thamani ya sh. milioni tano.


MWISHO.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: