Na.WAF-Mbeya


Wizara ya Afya kwa kushirikiana na asasi ya AGENDA imewataka wataalamu wa Afya ya kinywa na meno kutokuziba meno bila kutumia dawa yenye madini ya zebaki ijulikanayo kama Amalgma kutokana na kuwa na athari kwa binaadamu. 


Wito huo umetolewa leo na Afisa kutoka Idara ya tiba-Wizara ya Afya,sehemu ya kinywa na meno Dkt. Msafiri Kabulwa  wakati wa mafunzo kwa wataalamu wa afya ya kinywa na meno juu ya kuziba meno kwa kutumia kemikali zisizo na madini ya zebaki yaliyofanyika jijini Mbeya.


Dkt. Msafiri amesema Zebaki ina athari kubwa kwenye  mazingira na afya ya binaadamu, pia ina uwezo wa kuharibu ukuaji wa ubongo wa mtoto tangu akiwa tumboni kwa mama


"Zebaki huweza kutoka kwa mama mjamzito na kuingia kwa mtoto aliye tumboni wakati wa ujauzito, ama  kupitia maziwa ya mama wakati wa kunyonyesha na kuleta athari katika ukuaji wa ubongo wa mtoto."Amesema Dkt. Msafiri


"Athari za ukuaji wa ubongo ni pamoja na kuharibu uwezo wa mtoto wa kufikiri na hatimaye kumfanya mtoto ashindwe kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi hapo baadaye" Amesema Dkt. Msafiri


Aidha, Dkt. Msafiri amesema wizara imelenga kuikinga jamii dhidi ya madhara yatokanayo na madini ya zebaki kwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kuzibia meno zisizokuwa na madini ya zebaki kupitia bohari ya dawa(MSD)


"Kemikali za kuzibia meno zisizokuwa na madini ya zebaki zinapatikana hapa nchini kwa wasambazaji binafsi na kupitia bohari ya dawa (MSD)" Amesema Dkt. Msafiri


Naye, Afisa programu mwandamizi wa asasi ya AGENDA Bi. Dorah Swai amesema Mwaka 2013 Tanzania iliungana na nchi nyingine ulimwenguni kusaini Mkataba wa Kimataifa wenye lengo la kulinda afya na mazingira kutokana na athari za zebaki unaojulikana kama Mkataba wa Minamata wa Zebaki ambapo Tanzania iliridhia mkataba huo mwezi Oktoba 2019 na hivyo kuuzidishia nguvu ya utekelezwaji wake hapa nchini. 


"Kwa sasa ni juu ya wataalam wetu kuunga mkono juhudi hizo kwa kutimiza yale yote yalioainishwa kwenye mwongozo na kwenye kanuni, endapo walikuwa hawajaanza kufanya hivyo."Amesema BI. Dorah


Share To:

Post A Comment: