NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) kutolea macho miradi 36 ya maendeleo inayotekelezwa kupitia fedha zinazotokana na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) Mkoani Arusha.


Ndejembi ametoa agizo hilo wakati akizungumza na Waratibu wa TASAF kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha ambapo amewataka kusimamia kwa uadilifu miradi hiyo yenye thamani ya Sh Bilioni 3 inayotekelezwa ndani ya Mkoa huo.

Amesema litakua jambo la ajabu kuona watendaji hao wa TASAF wanashindwa kusimamia kwa uadilifu miradi hiyo ambayo Rais Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake ametoa kiasi kikubwa Cha fedha ili wananchi wake waweze kunufaika moja kwa moja.

" Mradi wa TASAF ndio mradi ambao unalenga maisha ya Watanzania wa hali ya chini moja kwa moja, na kwa mapenzi yake Mhe Rais ametoa kiasi cha Sh Bilioni 3 kwa ajili ya kutekeleza miradi 36 inayotokana na mahitaji ya kaya maskini kwenye Mkoa huu, hivyo niagize watendaji wa TASAF hapa Arusha kuisimamia miradi hii kwa uadilifu mkubwa.

Niagize TAKUKURU kusimamia na kuangalia kwa ukaribu miradi hii na haswa matumizi yake lakini niagize Halmashauri kufanya bulk procurement yaani wanunue vitu kwa pamoja badala ya kumpa mzabuni fedha anunue saruji, anunue nondo basi wanunue vitu vyote pamoja ili kuondoa gharama isiyo na tija," Amesema Naibu Waziri Ndejembi.

Naibu Waziri Ndejembi pia ametaka ushirikishwaji wa viongozi wengine akiwemo Mkuu wa Wilaya, Wabunge na Madiwani kwenye utekelezaji wa miradi hiyo ili waweze kuifahamu na kuifanyia ufuatiliaji pindi inapokua inatekelezwa.




Share To:

Post A Comment: