Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limemkamata, Mohamed Omary (27), mkazi wa Chamazi kwa tuhuma za kushiriki katika matukio ya unyang’anyi wa Pikipiki kwa waendesha Bodaboda kwa kushirikiana na wenzake, Athuman Abdallah (29), mkazi wa Yombo na Hassan Twaha maarufu kama 'Dangote' (21),


Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ACP Jumanne Muliro amesema mbinu ambayo wahalifu hao wamekuwa wakiitumia katika unyang’anyi wa Pikipiki ni kumtumia mwanamke mmoja ambaye hujifanya mjamzito aliyefahamika kwa jina la Aziza Hamza (21) Mkazi wa Yombo ambaye hukodi bodaboda mpaka walipo wenzake kwa ajili ya kupora pikipiki.


Amesema kuwa, tukio la uporaji likikamilika wahalifu hao huzipeleka pikipiki hizo kwa Omary Salum (30), Ndengereko, mkazi wa Tandika, Kilimahewa ambaye kazi yake ni kutoa GPRS/ ving’amuzi kwa pikipiki zenye ving’amuzi. Athuman Mohammed Bakari (42), mkazi wa Kilwa Kivinje yeye hujihusisha na kuzitafutia kadi na kuziuza katika mikoa ya Mtwara na Lindi.


Hata hivyo, Jeshi la Polisi limefanikiwa kumkamata Sophia Musa, miaka 28, mkazi wa Toangoma ambaye ndiye mpokea maombi ya kutengeneza kadi toka kwa Athumani Bakari na baadae kumpelekea Ibrahimu Ally (31), mkazi wa Buguruni ambaye hufanya kazi ya kudurufu kadi hizo za Pikipiki.


Katika katika upekuzi watuhumiwa hao wamekutwa na Pikipiki tatu (3) za wizi,ambazo ni MC 292 DC,MC 733CEG na MC 250 DBF, Kadi za pikipiki (9) Kadi za Gari (11), vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya kumaliza elimu ya sekondari, stika za mamlaka ya mapato (TRA) na stika za Baraza la Mitihani vyote vinachunguzwa.
Share To:

JUSLINE

Post A Comment: