Na Ahmed Mahmoud

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI-Tengeru)pamoja na wakala wa mbegu ASA imegundua mbegu za mchicha lishe wa akeri ambao unaelezwa kuwa na madini Zinki huku pia ukiimarisha nguvu za kiume kwa wanaume wenye changamoto hiyo.

Tari inaeleza kwamba changamoto ya upungufu wa damu, udumavu pamoja na uoni hafifu kwa watoto na wajawazito nchini linakwenda kumalizika baada ya kugundulika kwa mchicha huo.

Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na taasisi hiyo mchicha huo umegundulika kuwa unaprotini asilimia 14.5 huku ukiwa ni chanzo bora cha vitamini A, B, Zinki, madini ya chokaa, chumvi na folikasidi.

Akizungumza hivi karibuni jijini Arusha katika ziara ya Mafunzo ya Waandishi wa Habari kutoka Kanda ya Kaskazini iliyoratibiwa Tume ya Taifa ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu (COSTECH), Mtafiti Mwandamizi, Emmanuel Lasway kutoka TARI Tengeru amesema utafiti umebaini mchicha huo unakwenda kupunguza tatizo la upungufu wa damu pamoja udumavu endapo utatumiwa vizuri.

Amesema kuwa endapo matumizi ya mchicha huo yatazingatiwa na wajawazito, watoto na wanaume ambao wanakabiliwa na tatizo la nguvu za kiume itasaidia kumaliza changamoto hiyo na kuondokana na hali hiyo.

“Kwa wanaume tunawashauri kutumia nafaka ya mchicha wa akeri kutokana na namna ambavyo umefanyiwa utafiti wa kina na kubainika kusaidia kupunguza tatizo nguvu za kiume".

“Hivyo kwa wanaume wenye changamoto hiyo wataweza kuimarisha ndoa zao na kuboresha mfumo wa uzazi,” amesema Lasway.

Kwa mujibu wa mtafiti huyo mchicha huo wa maajabu huvunwa shambani na kisha mbegu zake husagwa na kuchanganya kwenye vyakula ili kuongeza virutubisho.

Aidha, ameongeza kuwa mchicha huo pia una lishe unachangia kiasi cha asilimia 50 hadi 102 ya folikasidi ukilinganisha na mahindi asilimia 15-46 na ngano asilimia 20 hadi 51.

IFAHAMU ASA TENGERU;

Usalama wa nchi yeyote ni usalama wa chakula. Wakati huohuo usalama wa chakula hujengwa na uwepo wa usalama na matumizi sahihi ya mbegu bora. Ukuaji wa sekta ya kilimo huenda sambamba na matumizi ya technolojia bora ikiwemo mbegu bora za Kilimo.


Serikali pia ilianzisha kwa makusudi kabisa wakala wa Taifa wa uzalishaji na uendelezaji wa mbegu za kilimo (ASA) ili kuhakikisha usalama wa chakula nchini unabaki mikononi mwa serikali kwa maana ya usalama wa mbegu. Kimsingi katika jukumu hili la uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za kilimo ASA kama taasisi ya serikali imeazimia kuhakikisha azma ya serikali kufika kwenye uchumi wa viwanda kupitia kilimo inatimia.

Majukumu ya ASA mbali na  kuhakikisha mbegu bora zinapatikana na kuwafikia wakulima kwa wakati na kwa bei iliyo nafuu, inajukumu pia la kuzinadi kwa nguvu mbegu zinazozalishwa na zinazotengenezwa na vituo vya utafiti.

ASA ina mikakati mingi katika kujikwamua kwenye changamoto mbalimbali zinazopunguza kasi ya maendeleo ya tasnia ya mbegu nchini, ikiwemo kutumia fursa mbalimbali Aidha pia wakala unajukumu kubwa la kufanya kazi na sekta binafsi hasa makampuni binafsi ya mbegu ili kuhakikisha uwepo wa ongezeko la upatikanaji wa mbegu bora kwa mkulima wa nchi hii na kupunguza changamoto ya ukosefu wa mbegu bora nchini.


Mashamba yake 9 ya mbegu yaliyotawanyika katika kanda zote za kilimo nchini. Moja ya jukumu la ASA ni kushirikiana na makampuni binafsi (Public-Private partinership) katika kuongeza kazi ya uzalishajiwa mbegu nchini.

Ili kukamilisha jukumu hili la kushirikiana na makampuni binafsi, baadhi ya makampuni hutumia rasilimali za ASA iliwemo ardhi, mashine za uchakataji wa mbegu na mitambo ili kuzalisha mbegu zao na kuziuza kwa wakulima, baadhi ya makampuni pamoja na wakulima wa mkataba huzalisha mbegu na kuiuzia ASA.

Baadhi ya makampuni hayo pia hununua mbegu za msingi kutoka ASA na kuzizalisha na baadaye kuziuza kwa wakulima, katika ubia huu na makampuni binafsi ASA pia inashirikiana katika kubadilishana uzoefu na kupeana elimu katika nyanja za uzalishaji, uchakataji na uhifadhi wa mbegu bora.


Aina hii ya ubia ni muhimu sana kwa maendeleo ya Tasniaya mbegu na Kilimo kwa ujumla. Hivyo, ASA ina fursa mbalimbali ambazo zinaweza kutumiwa na wadau mbalimbali katika Tasnia ya mbegu lengo likiwa ni kuongeza kasi ya uzalishaji wa mbegu bora nchini.



Share To:

Arusha Newsroom

Post A Comment: