Mtendaji wa kata ya Lifuma wilaya ya Ludewa mkoani Njombe Venant Lupagalo amewakamata na kuwaweka ndani wazazi 7 ambao watoto wao hawajaripoti shuleni kwaajili ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza ikiwa ni utekelezaji wa agizo la mkurugenzi wa halmashauri ya Ludewa pamoja na mkuu wa wilaya hiyo.

Hayo yameelezwa wakati wa kikao cha wadau wa elimu na kamati ya ushauri ya wilaya hiyo ambacho hufanyika kila mwaka kwa lengo la kujadili maendeleo ya elimu ndani ya wilaya hiyo.

“Kikao cha tarehe 22 mwezi wa pili ndicho kilicho tupa ridhaa ya kuwakamata,kwa maana ni baada ya kupata maagizo na mkurugenzi kwa watendaji wa kata wote”alisema Lupagalo

“Tuliandaa migambo kuwasaka wazazi wote 12 kwa ajili ya kujua ni namna gani watoto hawajaenda shule,tukawakamata na kuwaweka lock up kwenye ofisi ya kata na katika kupata sababu za mmoja mmoja ikaonekana wengi wa hawa wazazi walipeleka watoto sehemu mbali mbali ili wakafanye shughuli kwa ajili ya kujipatia kipato”aliongeza Lupagalo

Kwa mujibu wa ripoti ya wanafunzi waliotakiwa kuripoti shuleni kuanza kidato cha kwanza kwa kipindi hiki cha mwaka 2022 iliyosomwa na Afisa elimu Sekondari Mikael Hadu amesema wanafunzi 3350 walitakiwa kuanza kidato cha kwanza lakini walioripoti ni wanafunzi 2962 sawa na asilimia 88.4 huku wanafunzi 388 sawa na asilimia 11.6 mpaka sasa hawajaripoti katika shule zao.

Aidha mkuu wa wilaya hiyo Andrea Tsere amechukizwa na watendaji wa kata ambao wameonekana kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wasio ripoti na kutochukua hatua zozote huku akimpongeza mtendaji kata wa Lifuma.

“Kuna maeneo wanafunzi hawajaripoti shuleni bado tuna kazi ya kufanya,tulishasema wazazi wote ambao watoto wao hawajaripoti shuleni wachukuliwe hatua za kisheria”amesema Andrea Tsere

“Nimpongeze mtendaji wa kata ya Lifuma,hivi sasa watu saba wa Lifuma ambao watoto wao bado hawajaingia darasani wako Lock up”alisema Tsere

Share To:

Adery Masta

Post A Comment: