Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi


Na Thobias Mwanakatwe, Arusha


VYAMA vya siasa nchini vimeshauriwa kusimamia mchakato wa kuundwa wa tume huru ya uchaguzi kwa kuwa ndio msingi mkubwa utakaowezesha upatikanaji haraka wa katiba mpya.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi (pichani), alisema hayo jana katika mahojiano na gazeti jijini hapa kuhusu suala la katiba mpya ambalo vyama vya upinzani vimelishikia kidedea kutaka mchakato wake uanze.

"Vyama vya siasa na wadau wote wa kisiasa walione suala la kuwa na tume huru ya uchaguzi liwe ndio kipaumbele namba moja kwasababu tume huru ya uchaguzi ikipatikana itaharakisha upatikabaji wa katiba mpya kupitia wingi wa majority katika bunge ambacho ndio chombo kinachoweza kuisimamia serikali kwenye uanzishaji katiba mpya," alisema.

Muabhi alisema inashangaza kuona baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanasema hawaoni umuhimu wa tume huru ya uchaguzi kabla ya katiba mpya wakiamini katiba hiyo ndio inaweza kuvunja aina ya mifumo ya uchaguzi iliyopo hapa nchini wakati sio kweli.

Alisema katika mazingira kama haya ya kisiasa tuliyonayo hatuwezi kukaa na uona kwamba katiba ni muhimu kuliko tume huru ya uchaguzi ambayo ndio inasimamia haki na misingi yote ya amani na utulivu.

"Tume ya Uchaguzi ndio yenye kutoa maamuzi na kutangaza nafasi zote za uongozi wa kisiasa kuanzia ngazi ya chini hadi ya rais,kwa hiyo utekelezwaji wa haki na amani imebebwa kwa asilimia 80 na kutokuwa na tume huru ya uchaguzi kwasababu hapo ndio 'reaction' ya machafuko yanapoweza kuanza," alisema.

Aliongeza viongozi wa vyama vya siasa, wafuasi na wanachama wao inapofika wakati wa uchaguzi mkuu ambao husimamiwa na Tume ya Uchaguzi huwa wakiamini watafanya vizuri katika uchaguzi husika lakini matokeo yanapotangazwa na kuwa tofauti na matarajio yao wanaelekeza lawama kwa tume na hapo ndio unakuja umuhimu wa tume kuliko katiba mpya.

"Kutokuwa na Tume Huru ya Uchaguzi tulishawahi kushudia matokeo ya uchaguzi yakifutwa visiwani Zanzibar baada ya kubaini mgombea wa chama fulani ameshinda tofauti na mategemeo ya tume hali ambayo ilileta sintofahamu na kusababisha uvunjifu wa amani na kutopatikana kwa mwafaka wa kisiasa visiwani humo," alisema.

Alisema tukio hilo lililotokea Zanzibar limeleta somo zuri ya kuona ni namna gani tume huru ya uchaguzi inaweza kuwa ni suluhisho la migogoro ya kisiasa ambayo husababisha madhira kwa viongozi, wanachama na wananchi wa ujumla wa vyama vya siasa," alisema.

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: