Imeelezwa kuwa, Kampuni ya Peak Resources Ngualla (PRNG) itakayo jihusisha na uchimbaji wa madini ya teknolojia ya  Rare Earth Elements ipo katika hatua za mwisho za makubaliano na serikali ili ianze uchimbaji wa madini hayo.


Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa mara baada ya kutembelea eneo linalotarajiwa kufunguliwa mradi huo lililopo katika kijiji cha Ngwala wilaya ya Songwe.


Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wanakijiji wa Ngwala Dkt. Kiruswa amewatoa wasisi wananchi wa kijiji hicho ambao wana shauku kubwa ya kuona mradi huo unaanza uzalishaji ili wapate fursa mbalimbali za kiuchumi ambapo amesema kuwa, Serikali ipo katika hatua za mwisho za makubaliano na kampuni hiyo.


Aidha, Dkt. Kiruswa amesema mradi huo ukianza uzalishaji utakinufaisha kijiji cha Ngwala na mkoa wa Songwe pamoja na taifa kwa ujumla kutokana na umuhimu wa madini hayo ambayo hutumika kutengenezea simu, vifaa vya umeme ikiwemo magari yanayo tumia umeme.


Pia, Dkt. Kiruswa amefanya mkutano na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika kijiji cha Saza ambapo amewataka wachimbaji wa madini hayo kuzingatia Sheria na Kanuni zilizowekwa na serikali ikiwa ni pamoja na kulipa kodi za serikali na kuachana na utoroshaji wa madini.


Naye, Mkuu wa Wilaya ya Songwe Simon Simalenga amesema, Kampuni ya  PRNG inashirikiana vizuri na jamii inayozunguka mradi ambapo hadi sasa kampuni hiyo haijaanza uzalishaji lakini imesaidia ujenzi wa madarasa, barabara pamoja na kituo cha afya kijijini hapo.


Pia, Simalenga amempongeza Naibu Waziri Dkt. Kiruswa kwa kufanya ziara katika wilaya hiyo ambapo amesema wadau wa madini pamoja na wananchi wa wilaya ya Songwe wamefarijika kuona kiongozi wa ngazi ya juu katika Sekta ya Madini kuwatembelea.


"Tumefarijika sana kukuona kiongozi wa ngazi ya juu mwenye dhamana ya madini kuja kutembelea wilaya yetu ya Songwe, tunaamini ujio wako utasaidia kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta yetu ya madini ikiwemo suala la Kampuni ya PRNG kuruhusiwa kuanza uzalishaji ambayo imekaa kwa muda mrefu bila kuanza kazi," amesema Simalenga.

Share To:

Post A Comment: