Moses Mashalla,Arusha 


Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha,Maximillan Iranqe amewataka waganga wanaojishughulisha na tiba asilia mkoani Arusha kuwekeza zaidi katika tafiti za mimea inayotibu maradhi ya mbalimbali kama nchi za barani Asia hususani China.


Pia awataka waganga hao kujiepusha na vitendo vya utapeli ili kuipa sifa na hadhi taaluma hiyo tofauti na inavyozungunzwa kwa sasa.


Meya Huyo alitoa kauli hiyo Leo wakati alipoalikwa kuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa halmashauri kuu ya chama cha waganga na wakunga wa Tiba asilia(Chawatiata) kilichofanyika katika ofisi za Ccm wilayani Arusha.


Akifungua mkutano huo Mh,Mstahiki Iranqe aliwataka waganga hao kufikiria kuwekeza nguvu zaidi kwenye ubora wa dawa mbalimbali hususani mitishamba inayotibu maradhi mbalimbali.


"Fikirieni kuwekeza kwenye ubora wa madawa yenu hususani mitishamba kama wanavyofanya nchi za Asia kama China" alisema Iranqe 


Hatahivyo,aliwataka washiriki wa mkutano huo kuepuka vitendo vya utapeli na udanganyifu ili kuipa sifa taaluma hiyo huku akiwataka kuboresha mazingira ya maeneo wanayofanyia kazi pamoja na bidhaa wanazowapa wagonjwa.


"Lazima mjipambanue baina ya waganga wa kienyeji na tiba asilia acheni kufunga dawa kwenye magazeti lakini muwe smart(nadhifu)" alisema Mstahiki Meya Iranqe


Hatahivyo,makamu mwenyekiti wa Chama hicho,Kiondo Msangi  alimwambia mgeni rasmi kuwa chama chao mbali na kisajiliwa kisheria na kupewa leseni ya uendeshaji lakini wamekuwa wakifanya kazi kwenye mazingira magumu kutokana na baadhi ya wanachama kukamatwa hovyo na kutozwa adhabu kinyume na sheria.


Msangi alisema kwamba kuna kikundi cha baadhi ya watu kimekuwa kikizunguka mkoani Arusha na kuwashawishi na kuwapotosha  wajumbe kutojiunga na chama hicho kutokana na sababu zao binafsi na kuiomba serikali kukichukulia hatua.


Naye katibu wa chama hicho ,Kifumba  Mkombozi alisema kwamba chama chao kimekuwa kikishirikiana na serikali katika kuwafichua wapiga ramli chonganishi,majambazi na hata kukemea mauaji na watu wenye ulemavu wa ngozi na kuiomba serikali kuwaunga mkono.


Awali kaimu mganga mkuu wa hospitali ya Mkoa wa Arusha (Mt Meru),Dk Omary Chande aliwataka waganga kuhakikisha wanawakamata wale wanaofanya shughuli za tiba asilia bila leseni kwa kuwa hao ndio wanachafua taaluma hiyo.


Dk Chande aliwataka washiriki hao pia   kuunga mkono na kuhamasisha  zoezi la chanjo ya Uviko -19 linaloendelea nchini  kwa kuwa wao wana nafasi kubwa ndani ya jamii.


Share To:

Post A Comment: