Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Innocent Bashungwa ameagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatoa kwa wakati posho za madaraka kwa Watendaji wa Kata ili ziwasaidie kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Waziri Bashungwa ametoa maelekezo hayo leo Februari 23, 2022 katika kikao cha  Baraza la Madiwani wilayani Karagwe kilichofanyika ukumbi wa Agaza, Karagwe, mkoani Kagera.

“Mheshimiwa Rais kwa kutambua  kazi nzuri wanayofanya watendaji wa kata kote nchini aliamua kuwawezesha kwa kutoa posho ya madaraka, hiyo posho sio kwa hisani ipo kisheria, naelekeza halmashauri zote nchini kuhakikisha kila mwisho wa mwezi wanatoa posho ya madaraka kwa wakati na ziwakute walipo,” amesema Waziri Bashungwa.

Aidha, Waziri Bashungwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya Karagwe, Julieth Binyura kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa kuhakikisha anasimamia na kumaliza migogoro ya ardhi ambayo imekithiri katika Wilaya hiyo na kusababisha umasikini kwa wananchi.

Akizungumzia upungufu wa walimu wa sayansi nchini, Waziri Bashungwa amesema ili kupunguza uhaba huo kwenye kibali cha ajira za walimu kitakachotolewa na Rais, walimu wa sayansi watapewa kipaumbele na mpango huo utaenda sambamba na ujenzi wa mahabara katika shule za sekondari na matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari

Waziri Bashungwa ameeleza kuwa malengo ya Wilaya ya Karagwe ni kuwa na Shule tatu za kidato cha tano na sita hivyo ifikapo Aprili mwaka huu Serikali itatoa fedha kukamilisha shule za sekondari za Kituntu na Nyabiyonza.

Pamoja na hayo, ameuagiza Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) wilayani humo kuhakikisha  wanaweka taa za barabarani kwenye barabara za mitaani wanazotengeneza.

“Barabara ya Nyakahanga kwenda Benako mkandarasi tayari amesaini mkataba wa kilometa  60, barabara ya Omurushaka hadi Nkwenda ipo katika hatua za mwisho mkandarasi kusaini mkataba na barabara ya Omugakorongo hadi  Murongo usanifu umekamilika

Vile vile, Waziri Bashungwa amesisitiza ukusanyaji wa mapato katika halmashauri uendane na  malengo yaliyowekwa huku wakizingatia matumizi ya fedha katika miradi ya maendeleo iendane na matarajio yaliyowekwa.

Wakati huo huo, Waziri Bashungwa ametoa zawadi na vyeti kwa wanafunzi na shule za msingi na sekondari zilizofanya vizuri katika mitiani ya mwaka 2021 na ameahidi kuendelea kufanya hivyo kila mwaka.

Share To:

Post A Comment: