Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Kakoso, imeitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha asilimia 40 inayopatikana kwenye mapato ya mamlaka hiyo inatumika kuboresha miundombinu ya bandari ili kuifanya bandari kuwa na ufanisi.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi ya uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso, amesema maboresho ya miundombinu yataongeza mapato na kuongeza matumizi ya bandari hiyo kwa Tanzania na nchi jirani.

“Tunatamani bandari hii iwe ya kwanza Afrika Mashariki kwani uwekezaji unaofanywa kwa sasa ni mkubwa na lazima iwe shindani na kuwe na tija kwa maboresho yanayofanywa na mnaweza kuongezea ile asilimia 40 ambayo iko kisheria kuboresha zaidi”,amesema Mwenyekiti Kakoso.

Aidha, Mwenyekiti Kakoso ameitaka TPA kuangalia upya eneo la mafunzo hasa kwenye TEHAMA ili kwenda na wakati hasa nyakati hizi ambazo teknolojia imerahisisha utoaji wa huduma mbalimbali katika mifumo ya bandari.

Mwenyekiti  Kakoso ametanaibaisha umuhimu wa TPA kuangalia maslahi ya watumishi ili kupunguza vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara kwa watumishi wa Mamlaka.

“Bado kunaonekana kuna viashiria vya vitendo vya rushwa katika Mamlaka, Mkurugenzi Mkuu aangalie namna ambavyo watumishi wanaweza kuongezewa mishahara ili kupunguza tamaa za kuomba rushwa maana mnazalisha fedha nyingi bila mishahara mizuri itakuwa changamoto", amesisitiza Mwenyekiti Kakoso.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, (Sekta ya Uchukuzi), amemuhakikishia Mwenyekiti Kakoso kuwa Wizara imejipanga vizuri kuhakikisha miradi yote ya bandari inasimamiwa vizuri ili kuongeza ufanisi wa bandari hizo.

Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Karim Mataka, amesema Mamlaka inaendelea kusimamia kwa karibu miradi yote ili ilete mabadiliko yenye tija kwa taifa na hatimaye kuchangia kwenye pato la Taifa.

Mhandisi Mataka ameongeza kuwa kwa sasa kazi kubwa inayofanyika ni kuwasimamia wakandarasi wa miradi yote ya bandari ili wakamilishe miradi hiyo kwa wakati na viwango.

Maboresho ya mradi wa upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam umeonesha matokeo ikiwemo kupungua  kwa ajali kutoka 5 mpaka kuziondoa kabisa, utiaji nanga wa meli 3 za mzigo kwa wakati mmoja na gati 0 mpaka 3 kuweza kuwa na nafasi ya kushushwa kwa magari zaid ya 3,000 kwa wakati mmoja.


Share To:

Post A Comment: