Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kuhakikisha wanazingatia utoaji huduma bora kwa wateja ili kuondoa malalamiko kwa wanaokwenda kupata huduma kwenye ofisi za ardhi.


Aidha, Ridhiwani aliwataka watendaji wa sekta hiyo ya ardhi nchini kufanya kazi kwa kuzingatia taaluma zao na kuacha kufanya kazi kwa kisingizo cha kutekeleza maagizo ya wanasiasa.


Naibu Waziri Ridhiwani alisema hayo mwishoni mwa juma alipokuwa akifunga kikao kazi cha menejimenti, wakurugenzi wasaidizi wa Wizara ya Ardhi pamoja na makamishna wa ardhi wasaidizi wa mikoa kilichofanyika mkoani Arusha.


‘’Wakati mnafikiria kutoa huduma kwa wananchi wetu, ‘customer care’ ni jambo la muhimu sana maana yapo baadhi ya malalamiko kutoka kwa wananchi wetu kuhusu ucheleweshaji wa makusudi wa kupatiwa huduma, suala ambalo kama watendaji wakuu tulipaswa kulishughulikia,’’ alisema Ridhiwani.


Naibu waziri huyo amewakumbusha watendaji hao wa ardhi kuwa, wizara ya Ardhi inakusanya mapato yake kutokana na kodi ya pango la ardhi na kuwataka chanzo hicho kilindwe kwa kuwajali wateja na kiendane na utoaji hati za ardhi.


Share To:

Post A Comment: