WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inaangalia utaratibu utakaofaa kuhusu suala la uhifadhi katika eneo la Loliondo lililopo kwenye wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.

 

"Katika mjadala wetu wa leo, mmetoa maoni nasi tumeyapokea. Bado Serikali inayaangalia maslahi mapana ya umma. Tutawashirikisha pia ni lipi lina maslahi mapana kwa Watanzania."

 

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Februari 14, 2022) wakati akizungumza na wadau wa uhifadhi kwenye kikao kilichofanyika Wasso-Loliondo. Amesema Serikali imepokea maoni waliyoyatoa, yatayojumuishwa na kuyawasilishwa kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. 

 

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema alichoenda kufanya leo ni utekelezaji wa ushauri uliotolewa na wabunge kwa Serikali kupitia Mwenyekiti wa Kamati wa Maliasili na Utalii iliyoielekeza Serikali iende katika maeneo ya Loliondo, Ngorongoro na Sale na kuzungumza na wananchi.

 

“Kama ambavyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza lazima tuimarishe utalii na kuhakikisha wananchi wanashirikishwa, Waheshimiwa wabunge ambao ndio wawakilishi wametoa maoni yao ikiwemo kushauri suala la ushirikishwaji na ndio maana leo nimekuja hapa kuwasikiliza”.

 

Waziri Mkuu amesema wote tunatambua kuwa idadi ya watu na mifugo imeongezeka ndani ya hifadhi ambapo tusipotafuta suluhisho la kudumu hifadhi zetu zitaathirika. “Sisi sote tunatambua eneo hili ni la utalii, lazima tufike mahali tuamue kama tunataka utalii au la," amesema. 

 

Waziri Mkuu amesema amefarijika kusikia kwamba wachangiaji wote waliozungumza hakuna aliyesema ardhi ni yao. "Kati ya mambo yamenifariji, sijasikia mtu akisema ardhi yetu, ardhi yetu. Sote tunatambua kuwa ardhi iliyo ndani ya mipaka ya nchi hii ni ya umma lakini tumeikasimu kwa Mheshimiwa Rais kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania."

 

Katika kikao hicho, wananchi wa makundi mbalimbali walipewa nafasi kutoa maoni yao wakiwemo mbunge, madiwani, malaigwanan, wanamije (batemi) na wenyeviti wa vijiji. Katika maoni yao, wengi wao walisema wako tayari kushirikiana na Serikali kuendelea kutunza rasilimali za Taifa.

 

Waliomba wapatiwe elimu ya uzazi wa mpango, wapimiwe ardhi za vijiji ili kupunguza migogoro inayojitokeza mara kwa mara. Wilaya ya Ngorongoro ina tarafa tatu za Loliondo, Sale na Ngorongoro.

Share To:

Post A Comment: