Mwandishi wetu,


Mkuu wa wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara,Seleman Serera ameagiza wanafunzi wote wa shule za msingi wilayani humo ambao hawana sare za shule waruhusiwe kuhudhuria masomo mara moja na wasizuiwe.


Serera ametoa kauli hiyo Leo wakati alipofanya ziara ya kutembelea shule mbalimbali za msingi wilayani humo wakati akisimamia zoezi la ugawaji wa vyakula vya wanafunzi katika baadhi ya shule.


Zoezi la ugawaji wa vyakula hivyo liliratibiwa na shirika la maendeleo la Eclat Foundation lililopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara.


Akizungumza katika shule ya msingi Nadonjuki Serera alitoa maagizo kwa wakuu wa shule za msingi wilayani humo kutowazuia wanafunzi wasio na sare kuingia darasani bila kuzuiwa.


"Watoto wote hata wale wasio na sare wakubaliwe kuingia darasani wakati wazazi wamajipanga" alisema Serera 


Serera alisisitiza kwamba  asilimia kubwa ya wazazi katika wilaya ya Simanjiro wamekumbwa na tatizo la ukame hali iliyopelekea kukosa kipato na hata kumudu michango ya kugharamia chakula mashuleni.


Hatahivyo,mkurugenzi wa shirika la maendeleo la Eclat Foundation, Peter Ole Toima alisema kwamba kutokana na ukame wananchi wengi wa maeneo ya wafugaji wamepitia kipindi kigumu hususani  kupoteza mifugo mingi kutokana na kukosa malisho.


Ole Toima alisisitiza kwamba shirika lao limeona changamoto hiyo na hivyo kuamua kuwashika mkono kwa kuwapatia wanafunzi mbalimbali vyakula lengo likiwa ni kuongeza mahudhurio shuleni sanjari na kuongeza kiwango cha ufaulu.


"Lakini wazazi tutakuwa tumewaokoa katika suala la michango ya vyakula mashuleni kwa kuwa wengi wamekabiliwa na ukame na wamepoteza mifugo mingi kutokana na ukame" alisema Ole Toima


Jumla ya magunia 251 ya mahindi na maharage yamekabidhiwa Leo na shirika la Eclat Foundation katika shule tatu za msingi na moja ya sekondari wilayani Simanjiro ambapo chakula hicho kinataraji kuwasaidia wanafunzi katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Share To:

Post A Comment: