Mbunge wa Jimbo la Rombo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda Januari 23, 2022 amezindua mashindano ya Ligi ya Mbunge Cup Kwa vijana wa Rombo ikiwa ni sehemu ya maadhinisho ya kumbukizi ya miaka 45 ya kuzaliwa  kwa Chama cha Mapinduzi.


Akizungunza kabla ya uzinduzi huo katika kiwanja cha mpira cha Sabasaba kilichopo wilayani Rombo Prof. Mkenda amesema Serikali ya CCM imefanya mambo mengi ya maendeleo nchini baada ya  kupata Uhuru, hivyo amewataka vijana hao kujivunia mafanikio hayo ambayo yamepatikana chini ya uongozi wa chama hicho.


Amesema Serikali imefanya kazi kubwa  ya kuboresha sekta mbalimbali huku akitolea mfano uboreshaji mkubwa wa miundombinu ya barabara katika mikoa yote nchini kuanzia barabara za mikoa, wilaya, vijijini  na mitaa ambapo imetumia fedha nyingi kwa ajili ya miundombinu hiyo, huku akiwataka wanarombo kuhakikisha wanailinda miundombinu hiyo kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.


"Wakati nasoma miaka ile miundombinu ya barabara Rombo ilikuwa mibaya sana. Kwa wakati ule ili uweze kufika safari yako ilikuwa ni lazima kusubiri basi saa tisa alfajiri lakini leo usafiri upo wakutosha  na tunaona magari madogo yanafika hapa bila shida, hili ni jambo la kujivunia sana, niwasihi ndugu zangu tuilinde miundombinu hii ili itufae sisi na vizazi vyetu," amesisitiza Prof. Mkenda.


Mbunge huyo kabla ya kuzindua mashindano hayo pia alizindua shina la wakereketwa la vijana wa bodaboda Chato lililopo wilayani humo ambapo amewataka vijana hao kuendesha bodaboda kwa kufuata sheria za barabarani  kwa ajili ya  usalama wao na abiria wanaowabeba.


Aidha, amewataka vijana waendesha bodaboda wilayani humo kujiunga katika vikundi ili iwe rahisi kwa Serikali kutatua changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa shughuli zao huku akiahidi kushirikiana nao kama Mbunge.


Mbunge huyo pia  amekagua ujenzi wa nyumba inayojengwa na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Rombo ambayo itatumika kwa ajili za umoja huo.


Shughuli zote zimeandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi wa Wilaya  ya Rombo ikiwa ni sehemu ya  Maadhimisho ya Kumbukizi ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa Chama hicho.

Share To:

Post A Comment: