Na. Angela Msimbira, Njombe


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amemuagiza  Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za  Vijijini  na Mijini  (TARURA), Mhandisi Victor Seff kuwaorodhesha  makandarasi  wote ambao wako kwenye rekodi ya kutokufanya vizuri  na wababaishaji kufutwa na kutofanya kazi za TARURA nchi nzima.


Ameyasema hayo mapema leo wakati akikagua barabara ya Igosi –Ujindile-Wangama yenye urefu  wa kilometa 16.9 iliyopo kata ya Wangama katika Halmashauri ya Wilaya  ya Wanging’ombe Mkoani Njombe ambayo inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha changarawe kutokana na Fedha za Tozo ya Mafuta.


Waziri Bashungwa amesema  kuwa Makandarasi ambao hawafanyi vizuri wasiwe wanahamishwa kutoka sehemu  moja hadi nyingine, badala yake wapewe kazi  makandarasi ambao wanauwezo wa kufanya kazi kwa viwango na kasi inayotakiwa.


“Serikali ya Awamu ya Sita inataka  kupeleka huduma kwa wananchi kwa kuboresha mawasiliano ya miundombinu ya barabara hasa vijijini, Rais wetu anataka kuiboresha TARURA  ili iweze kuhudumia watanzania, Makandarasi wanaofanya kazi kwa mazoea  hawahitajiki kwa sasa “, amesema Waziri Bashungwa


Waziri Bashungwa amesisitiza kuwa moja ya vitu ambavyo vitafanyika kwa  Makampuni na Makandarasi wazembe na rekodi zinaonyesha ni wazembe  ameelekeza apelekewe taarifa zao ili wasipatiwe kazi za TARURA kwani Serikali itafanya kazi na Makandarasi watakaofanya kazi kwa weledi na kukamilisha  miradi kwa wakati  na ameelekeza kuwepo kwa kanzidata kwa ajili ya Makampuni na Makandarasi ambayo yanafanya kazi vizuri ili waweze kupatiwa kazi za TARURA.


Amesisitiza kuwa lengo la kuanzishwa kwa TARURA nchini ni kuhakikisha  inawasaidia wananchi wa vijijini katika Suala zima la ujenzi wa miundombinu ya barabara ili kuwasaidia watanzania ambao ni wakulima kuwafungulia fursa za kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi, hivyo  ni wajibu kutumia makandarasi  wanaofanya kazi kwa uaminifu na kuhakikisha miradi wanayopatiwa na Serikali inakamilika kwa wakati.


Akiwasilisha taarifa kuhusu ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Mhandisi Boniface  Kasambo ameeleza kuwa barabara ya Igosi-Ujindile-Wangama ni muhimu kwa wanachi  wa eneo hilo kwa kuwa inatumika kusafirisha mazao ya biashara ikiwemo parachichi, viazi na mbao kutoka  mashambani Kata ya Wangama na Igosi kupeleka katika masoko  ya Njombe Mji na Makambako kupitia barabara kuu ya Njombe -Makete.


Mhandisi Kasambo amesema ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kuanza hivi karibuni, umeidhinishiwa zaidi ya shilingi  milioni 400  na  utajumuisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe, kuchimba mifereji na kujenga makalati.

Share To:

Post A Comment: