Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Anthony Mavunde ameItaka Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea TA(TFRA) kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sheria ya Mbolea namba 9 ya Mwaka 2009 katika kutimiza wajibu wao.

 

Amesema, wizara yake itajitahidi kufanya kazi na kuwafanya watumishi kuwa watulivu kwa kuwapa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, “tuheshimiane katika misingi ya utu kwani kazi inapimwa kwa matokeo na si vitisho” Mavunde amesisitiza.

 

Amesema hayo leo Januari 21, 2022 alipokutana na kuzungumza na Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) katika kikao kifupi kilichofanyika katika ukumbi wa mamlaka hiyo Jijini Dar es Salaam.

 

Aliendelea kusema, ninyi ni damu yetu, ndio mnaosukuma gurudumu la Wizara ili lisonge mbele hivyo upendo na mshikamano ndio msingi wa utendaji wetu.

 

Aidha, Naibu Waziri Mavunde aliwataka wajumbe wa kikao hicho kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kufanikisha juhudi za wawekezaji wanaotarajia kujenga kiwanda cha mbolea cha itracom jijini Dodoma kwa kubaini endapo aina ya mbolea itakayozalishwa itaendana na aina ya udongo wa eneo hilo na kuwashauri ipasavyo ili uwekezaji wao uwe na tija.

 

Pamoja na hayo, aliitaka Mamlaka hiyo kubaini idadi ya wakulima wanaotumia mbolea katika kilimo chao kupitia mfumo wa kimtandao wa mbolea (Fertilizer Information System - FIS) ambao umefanikisha kutoa huduma za usafiri wa wafanyabiashara wa mbolea na utoaji wa leseni, vibali vya kutoa na kuingiza mbolea nchini pamoja na usajili wa mbolea.  

 

Akizungumzia kuhusu bei ya mbolea, Mavunde ameitaka mamlaka kuwakilisha ushauri wa kitaalamu utakaosaidia katika kumpunguzia mzigo wa gharama mkulima ili kumfanya afurahia uwekezaji anaoufanya kupitia kilimo na baadae kuondoa manung’uniko.

 

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dkt. Stephan Ngailo amesema moja ya jukumu kubwa la TFRA ni kudhibiti ubora na kusimamia biashara ya mbolea katika mnyororo wa thamani ikiwemo utengenezaji, uingizaji na uuzaji nje ya nchi, uhufadhi na usambazaji.

 

Akizungumzia jukumu la udhibiti ubora, Dkt Ngailo amesema TFRA imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti utengenezaji na uingizwaji wa mbolea zisizokuwa na ubora na kuhakikisha kwamba wakulima wanapata mbolea bora kwa wakati.

 

DKT. Ngailo amebainisha kuwa Tanzania ni nchi mojawapo barani Afrika Kusini mwa Jagwa la Sahara yenye matumizi madogo ya mbolea ambapo matumizi yake ni kilo 19 za virutubisho kwa hekta.

 

Amesema kiwango hiki ni kidogo ikilinganishwa na kiwango kilichowekwa na azimio la Maputo (The Maputo Declaration) la kuongeza  matumizi ya mbolea katika eneo la ukanda wa SADC kufikia kilo 50 za virutubisho kwa hekta ifikapo mwaka 2015 na kubainisha kuwa Tanzania inafanya juhudi na kuweka mikakati mbalimbali kwa lengo la kutekeleza Azimio hilo.

 

Dkt. Ngailo amesema kiasi cha tani 698,260 za mbolea zinakadiriwa kutumika kwa msimu wa mwaka 2021/2022 na kubainisha kuwa kuanzia Julai 2021 hadi Desemba 31, 2021 upatikanaji wa mbolea ulikuwa zaidi ya tani 409,232 sawa na asilimia 59 ya makadirio, amesema kati ya tani hizo, tani 117,900 ni bakaa ya  msimu wa 2020/21, tani 32,162 zimezalishwa ndani ya nchi ambapo jumla ya tani 43,175 ziliuzwa nje ya nchi na kufanya upatikanaji kwa ajili ya matumizi ya ndani kuwa tani 366,057 sawa na asilimia 52 ya mahitaji ya ndani ya nchi.

 

Ameongeza kuwa, kiasi cha tani 173,957 kiliuzwa ndani ya nchi na kufanya kiasi kilichobaki hadi kufikia Disemba 31, 2021 kuwa tani 192,100 sawa na asilimia 28 ya mahitaji ya ndani ya nchi. Kati ya kiasi hicho, tani 15,634 ni mbolea ya kupandia (DAP) na tani 51,845 ni mbolea ya kukuzia (UREA) na kukiri kuwa mbolea zinaendelea kupakuliwa bandari ya Dr es Salaam kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulini kote nchini.

 

Akizungumzia changamoto zinazoikabili mamlaka, Dkt. Ngailo alisema ni pamoja na kupanda kwa bei ya mbolea katika soko la dunia kulikosababisha bei ya mbolea zinazoingia nchini katika kipindi cha Julai hadi Disemba Mwaka 2021/2022 kupanda zikilinganishwa na bei za kipindi kama hiki Mwaka 2020/2021.

 

Changamoto nyingine zilizobainishwa ni pamoja na gharama kubwa za usambazaji wa mbolea nchini, uzalishaji mdogo wa mbolea katika viwanda vilivyopo nchini, matumizi madogo ya visaidizi vya mbolea.

 

Akizungumzia namna ya kutatua changamoto hizo, Dkt. Ngailo amesema ni pamoja na kuwajengea uwezo wataalam juu ya teknolojia mbalimbali mpya za mbolea, kuendelea kuimarisha udhibiti wa ubora wa mbolea nchini kwa kutoa mafunzo kwa wakaguzi wa mbolea kila halmashauri nchini, kusajili mbolea zote, watengenezaji na wauzaji wa mbolea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara sehemu zote ikiwa ni pamoja na bandarini, mipakani na madukani.

 

Aidha, Serikali kupitia TFRA inaratibu ujenzi wa maabara mahususi ya mbolea, kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uzalishaji wa mbolea na visaidizi vyake ndani ya nchi pamoja na kushirikiana na wadau katika kuhamamsisha matumizi ya visaidizi vya mbolea.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TFRA, Prof. Anthony Mshandete ameeleza mafanikio yaliyopatikana kupitia bodi yake kwa kipindi alipoteuliwa kusimamia mamlaka hiyo kuwa ni pamoja na kuisimamia mamlaka katika kuandaa na kusimamia Mpango Mkakati wa Taasisi (Corporate Strategic Plan) unaosaidia katika utekelezaji wa majukumu ya mamlaka.

 

Aidha, amemshukuru Naibu Waziri, Anthony Mvunde kwa kuchagua kutembelea Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania ikiwa ni taasisi ya kwanza iliyo chini ya Wizara ya Kilimo mara baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo

Share To:

Post A Comment: