Mchungaji Kiongozi wa Kanisa  la Moravian Parishi ya Sabasaba mkoani Singida, Samwel Ngamanja akitoa mbaraka kwa Waumini wa kanisa hilo baada ya kumaliza ibada iliyokwenda sanjari na maombi maalumu ya kumshukuru Mungu kwa kutupatia mvua yaliyofanyika leo. 
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa  la Moravian Parishi ya Sabasaba mkoani Singida, Samwel Ngamanja akizungumza kwenye ibada hiyo. Kushoto ni Msaidizi wa Mchungaji huyo Obedi Mwalwiba.
Mtumishi wa Mungu Anna Emmanuel akiongoza maombi hayo ya kumshukuru Mungu kwa kutupatia mvua na kuwaombea viongozi mbalimbali wa nchi yetu.
Maombi yakiendelea.

Unyenyekevu wakati wa maombi hayo.

Mchungaji Kiongozi wa Kanisa  la Moravian Parishi ya Sabasaba mkoani Singida, Samwel Ngamanja na Msaidizi wake Obedi Mwalwiba wakiomba kwenye maombi hayo.

Ibada ikiendelea.


Na Dotto Mwaibale, Singida


WAUMINI wa Kanisa  la Moravian Parishi ya Sabasaba mkoani Singida wamefanya maombi maalumu ya kumshukuru Mungu kwa kuleta mvua ambayo ilikuwa ikitishia nchi kwa ukame.

Akizungumza katika ibada ya maombi hayo Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo, Samwel Ngamanja alisema watanzania tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa upendo wake wa kutuletea mvua kwani kila mmoja wetu alikuwa na wasiwasi kutokana na tishio la ukame ambalo lilianza kujitokeza.

" Tulikuwa katika kipindi kigumu tukiwaza kupata mvua huku tukiwa katika tishio la kukosa chakula, mifugo kufa na vyanzo vya maji kuanza kukauka lakini kutokana na upendo wake mvua imeanza kunyesha" alisema Ngamanja.

Alisema wanacho muomba Mungu ni mvua hizi alizotupa ziwe za kawaida zisilete mafuriko na maafa na kuwa katika maeneo ambayo bado hawajaanza kuzipata wasiwe na wasiwasi kwani zitanyesha kwa uwezo wake.

Aidha Mchungaji Ngamanja alisema kukosekana kwa utii na mabishano dhidi ya watu wenye mamlaka kunasababisha kushindwa kuyafikia mafanikio na maendeleo ya nchi yetu hivyo kila mmoja wetu anapasa kuitii mamlaka ya nchi ambayo imewekwa na Mungu.

"Kila mmoja wetu kwa dini yake anapaswa kuitii mamlaka iliyopo kuanzia ngazi ya familia, nyumba za ibada na Taifa kwa ujumla bila  kuzimvunja amri 10 za Mungu.

Alisema maisha yetu yasio na radha wala thamani yanaweza kubadilishwa na Mungu na kuwa mazuri iwapo kila mmoja wetu atabadilika na kuacha kutenda dhambi na kutimiza kila jambo linalompendeza.

Waumini wa kanisa hilo kwa pamoja wakiongozwa na Mtumishi wa Mungu Anna Emmanuel walitumia ibada hiyo kuwaombea viongozi wa nchi yetu kuanzia Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Baraza la Mawaziri, Wabunge, wakuu wa mikoa na wengine wote ili waendelee kuongoza nchi huku wakiwa na hofu ya Mungu.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: