Na Joachim Nyambo,Chunya.


SERA bora ya uwekezaji nchini sambamba na Ushirikiano baina ya wadau mbalimbali wakiwemo utawala,walimu,wanafunzi pamoja na wazazi umetajwa kuwa siri ya mafanikio ya Shule ya mchepuo wa kingereza ya Holyland iliyopo Makongolosi wilayani Chunya mkoani Mbeya iliyoshika nafasi ya kwanza kitaifa kwenye matokeo ya darasa la nne 2021 kwenye kundi la shule zilizokuwa na watahiniwa chini ya 40.


Mwalimu Mkuu wa shule hiyo,Yona Mwakalinga alibainisha hayo alipozungumzia mafanikio iliyoyapata shule hiyo kwenye mtihani wa kitaifa wa darasa la nne ikiwa ni miongoni  mwa shule changa hapa nchini.


Mwalimu Mwakalinga alisema ilikuwa vigumu kwao kuamini kuwa wameshika nafasi ya kwanza kitaifa baada ya matokeo kutangazwa lakini waliporejea kwenye njia walizopita wakajiona walistahili kwakuwa kumekuwepo na ushirikiano mkubwa baina ya wadau wakiwemo viongozi wa kiserikali.


Alisema wazazi wa wanafunzi pia wamekuwa na mchango mkubwa kwa shule hiyo kwakuwa wamekuwa wakitoa ushauri kila walipokuwa wakiwatembelea watoto wao na hivyo kuwezesha mazingira ya wanafunzi kuzidi kuboreshwa hasa wakati wa kuelekea mtihani.


"Sasa tumeamini kuwa ushirikiano ni silaha muhimu sana...Utawala unashairikiana na walimu kwa kuhakikisha maslahi kwa wakati...wazazi wanatoa ushauri wanapotutembelea..wanafunzi walikuwa na utayari wa kuendana na ratiba ya vipindi..lakini pia ushirikiano mkubwa wa viongozi wa serikali nao ulikuwa na msukumo mkubwa na wenye kututia moyo." alisema mwalimu Mwakalinga.


Kwa upande wake mwalimu wa taaluma wa shule hiyo,Mwalimu Ally Nashon alisema kufanya kazi kama timu ni jambo muhimu kwenye Taasisi yoyote iliyolenga kupiga hatua kwenye mafanikio kama ilivyotokea kwa shule yao.


Mwalimu Nashon alisema matokeo mazuri waliyoyapata yanawapa kazi nyingine ya kuhakikisha wanakuwa na mipango madhubuti ya kuendeleza juhudi na mapambano ili kutunza heshima waliyoipata kwa mitihani ya kitaifa mingine ijayo.


Mkurugenzi mkuu wa shule ya Holyland,Lawena Nsonda maarufu kama Baba mzazi alisema matokeo hayo mazuri yanaupa moyo utawala wa kuona uwekezaji walioufanya ni jambo lililo na manufaa makubwa zaidi ya walivyofikiri awali.


"Sasa tumeona kuwa kweli hakuna jambo dogo..na unaweza ukona kitu unachofanya ni kidogo kumbe kina uzito mkubwa ndani ya jamii.Tumejikuta tunapokea simu nyingi na tunapokea wageni wengi."

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: