Na Teddy Kilanga,Arusha

Halmashauri ya Arusha iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha imeanza kuweka mikakati ya kuwafuatilia wazazi ambao hawajapeleka shule wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza ili kuwachukulia hatua cha kisheria.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,Mkurugenzi wa halmazhauri hiyo,Suleiman Msumi alisema kati ya wanafunzi 7890 walioripoti shule ni 4258 ambaye ni sawa na asilimia 51 hivyo ni vyema wazazi na walezi wakawapeleka shule kwani serikali imehimarisha miundombinu ya madarasa na viti vya kukalia shuleni.

"Mikakati ya kuwafuatilia wanafunzi ambao hajaripoti shule walizopangiwa ni pamoja na kutumia watendaji wa vijiji kwenda nyumba kwa nyumba ili kuwabaina wazazi na walezi ambao hawajawapeleka watoto wao shule kuwachukulia hatua za kisheria,"alisema Mkurugenzi Msumi.

Msumi alisema wazazi na walezi wanatakiwa kutekeleza wajibu wao wa kuwapeleka watoto shule bila kushurutishwa kwani lengo la serikali ni kumtoa Mtanzania kwa leo na kesho katika adui ujinga kwani ni moja ya maadui tangu mwaka1961 wanapambana nao.

Aidha alisisitiza kuwa viongozi wote kuanzia ngazi za vijiji hadi kata kusimama katika hilo kuhakikisha kwamba kwenye maeneo yao wanafunzi waliofaulu wahakikishe wanaenda shule na itakapofika muda wa kuripoti kuisha inabidi sheria ichukue mkondo wake.

"Mimi kama Mkurugenzi Mtendaji sitakuwa na simile kwa mzazi au mlezi yeyote atakayemficha mtoto ndani kwa ajili ya  masuala ya mila na desturi au muda wa kwenda shule mwanafunzi anakwenda kuchunga ng'ombe na wengine kuhozeshwa nawahakikishia tutawafuatilia nyumba hadi nyumba,"alisema Msumi.

Alisema msako huo wa nyumba kwa nyumba utapitia majina yote ya wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza kuwafuatilia ili kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa mzazi au mlezi aliyekaidi agizo la serikali la kuwapeleka watoto shule.
Aidha aliongeza kuwa serikali imeshaboresha miundombinu ya madarasa pamoja na viti ili kuondoa adha ya wananchi kuchangia alafu inatokea mzazi anakuwa sehemu ya kukwamisha ndoto ya mwanafunzi kutokwenda shule.

Share To:

Post A Comment: