Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt. Tulia Ackson, amewatembelea na kuwapa pole Wananchi wa mtaa wa Itezi mashariki, Kata ya Nsalaga iliyo Jijini humo ambao wamekumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua.


Pamoja na yote, Dkt. Tulia ameahidi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya kuhakikisha wanaboresha mazingira ya miundombinu huku akiwataka Wananchi nao kutoa ushirikiano wao. 


“Leo tumekuja kuona adhari zilizojitokeza ili tuweze kuona ni namna gani tutaweza kuzitatua, tumeambatana na Mkuu wa Wilaya, Mstahiki Meya, Watu wa TARURA pamoja na watu wa Idara ya maji ili tuweze kupata suluhu ya tatizo hili. Tunafahamu wote kwamba Rais wetu anaitwa Samia Suluhu basi muwe na Imani kwamba Suluhu imeshapatikana”- Dkt. Tulia Ackson

“Siku ya Jumatatu itakuja timu ya wataalamu ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa chanzo cha tatizo, Lakini ndugu zangu hapa tumeona changamoto moja…! kumekuwa na kilimo mpaka pembezoni kabisa mwa kingo za mto, niwaombe sana tuache tabia hii mara moja kwasababu inasababisha mto kuendelea kutanuka na kufanya maji kuacha njia na mwisho wa siku kuleta athari kama hizi”- Dkt. Tulia Ackson


“Nimeona baadhi ya Wananchi hapa nyumba zao zimekumbwa na athari kubwa zaidi ikiwemo kusombwa kwa vitu vyote ndani, Mimi Mbunge wenu nimeguswa katika hili na nitaleta mchele kilo 100 pamoja na maharage na nitamkabidhi Mwenyekiti wa mtaa kwakuwa ndio anafahamu zaidi waathirika ili aweze kugawa kwa wahanga husika lakini bado nitaendelea kushirikiana nanyi hadi mwisho wa jambo hili”-Dkt. Tulia Ackson


Nao Wananchi wa Kata hiyo Wamemshukuru Dkt. Tulia Ackson kwa namna ambavyo amekuwa akijitoa kila mara na kushirikiana nao katika kutatua changamoto mbalimbali zinazokuwa zikiwakabili.

Share To:

Post A Comment: