Geofrey Meena na Tito Mselem


Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inaongeza mchango wake katika pato la Taifa kupitia makusanyo ya Serikali, ajira kwa Watanzania na biashara zitokanazo na shughuli za madini.


Dkt. Biteko ametoa wito huo alipokuwa akizundua Bodi Mpya ya Wakurugenzi wa STAMICO uliofanyika jijini Dodoma ambapo amewaahidi ushirikiano pale utakapohitajika ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kulifanya Shirika hilo litimize malengo yake.


“Ilikuwa vigumu sana kwangu na wasaidizi wangu kuona nani wa kumuacha na nani wa kumchukua kwa kuzingatia kuwa wote walifanya kazi nzuri kwa Bodi iliyo pita, kazi yenu nzuri ilibadilisha sura ya Shirika hili na kutuletea heshima kubwa sisi kama Wizara ya Madini,” amesema Dkt. Biteko.


Dkt. Biteko amesema kazi iliyofanywa na Bodi ya Wakurugenzi iliyoisha muda wake imedhihirisha uwezo wao mkubwa na uzalendo wao katika kuleta maendeleo ya nchi na kuitaka Bodi mpya kuwa wasimamizi wazuri wa Shirika hilo kwa manufaa ya taifa.


Aidha, Dkt. Biteko ameipongeza menejimenti ya STAMICO kwa kuvuka lengo la makusanyo kwa miaka miwili mfululizo ambapo Mwaka wa Fedha 2019/20 Shirika lilivuka lengo kwa asilimia 120 na Mwakawa Fedha 2020/21 Shirika lilivuka lengo kwa asilimia 101.


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameipongeza STAMICO kwa hatua walio ifikia na kuwataka waendelee kulisimamia Shirika hilo ili kuhakikisha linafikia mipango wake iliyojiwekea na hatimaye Shirika liweze kuongeza kiwango cha gawio kwa Serikali.


Pamoja mambo mengine, Dkt. Kiruswa ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteuwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Madini ambapo ameahidi kufanya kazi kwa bidii na kwa uaminifu mkubwa.

Share To:

Post A Comment: