Wataalamu kutoka chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) wakiwa katika matayarisho ya awali ya kazi ya urasimishaji makazi holela katika mji mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya mwishoni mwa wiki.

Mkuu wa Cho cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Huruma Lugalla (Kushoto) akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wataalam wakati wa maandalizi ya awali ya urasimishaji makazi holela kwenye mji mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya mwishoni mwa wiki.

Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Huruma Lugalla (wa pili kulia) akikagua sehemu ya vigingi vitakavyotumika kwenye zoezi la urasimishaji makazi holela katika mji mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya mwishoni mwa wiki.

Mkuu wa Cho cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Huruma Lugalla (wa pili kulia) akitoa maelekezo wakati wa kutafuta alama eneo la Lumbila kata ya Luanda wilaya ya mbozi mkoani Mbeya kabla ya kuanza zoezi la urasimishaji makazi kwenye mji mdogo wa Mbalizi mwishoni mwa wiki. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)

******************

Na Munir Shemweta, WANMM MBEYA

Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kinatarajiwa kuanza kazi ya kurasimisha makazi holela katika mji mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya.

Kazi hiyo ni utekelezaji wa program ya Kupanga, Kupima na kumilikisha ardhi ambapo Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan iliipatia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi shilingi bilioni 50 kwa ajili ya kuzikopesha halmashauri 55 nchini.

Akizungumza jijini Mbeya mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro Huruma Lugalla alisema kiasi cha shilingi bilioni 1.2 zitatumika kwenye kazi hiyo na malengo ya chuo chake ni kukamalisha kazi hiyo kufikia katikati ya mwezi April 2022.

‘’Malengo yetu kazi hii ikamilike katikati ya mwezi April 2022 kwa kukamilisha kupanga na kupima viwanja vyote 35000 pengine nusu ya ya viwanja hivyo viwe vimefanyiwa utaratibu wa kumilikishwa’ alisema Lugalla.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Chuo cha Ardhi Morogoro, iwapo kazi hiyo itakamilika kwa wakati watakuwa wameisadia serikali na wananchi wa Mbalizi kupata maeneo yaliyopangwa na kupimwa sambamba na kuwa na umiliki wa uhakika.

Lugalla aliongeza kuwa, mikakati ya chuo chake cha ARIMO ni kukamilisha miradi yake yote ya urasimishaji kwa wakati sambamba na kuwasaidia wananchi kupata hati ili wazitumie kwa shughuli za maendeleo huku serikali nayo ikipata mapato kupitia kodi ya pango la ardhi.

‘’Pamoja na kazi ya hapa Mbalizi lakini tumefanya kazi pia katika jiji la Arusha kata ya Muriet ambako tumepima viwanja 20,222 na pia tumefanya Dar es Salaam kata ya Kivule tulikopima viwanja 30140 na zoezi linaloendelea ni kupata uidhinishaji kwa baadhi ya viwanja kutoka ofisi ya ardhi mkoa’’ alisema Lugala

Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo wa Urasimishaji Makazi Holela eneo la Mbalizi Manyama Majogolo alisema, tayari timu ya wataalam tayari imefika Mbalizi mkoani Mbeya kwa matayarisho ya awali kabla ya kuanza rasmi kazi katika eneo la mji mdogo wa Mbalizi.

‘’Kazi hizi za awali zikikamilika tunatarajia kuingia uwandani Januari 10, 2022 na kwa hivi sasa pamoja na maandalizi mengine pia tumeanza kuandaa vigingi na timu imesambaa kila eneo kuhakikisha tunaratibu vizuri maana nina imani tukianza vizuri tutamaliza vizuri ‘’ alisema Majogolo

Akielezea namna walivyojipanga kuhakikisha zoezi linakuwa na mafanikio, Majogolo alisema kuwa, wameanza kwa kuhamasisha wananchi kushiriki katika mradi huo ambapo katika uhamasishaji huo wameshirikisha pia viongozi wa serikali za mitaa, kata, mabalozi na ofsi ya halmashauri ili elimu iweze kuwafikia wananchi kwa ujumla wake.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: