WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema jukumu la kulea watoto na kutafuta mahitaji ni la wazazi lakini wajibu wa kuwasomesha watoto hao ni wa Serikali.

 

“Tulishasema, mtoto wa Kitanzania kwenda shule ni lazima. Watoto ni wao, lakini kwenda shule ni lazima. Ndiyo maana Serikali ilifuta ada katika shule zote.”

 

Alitoa kauli hiyo jana mchana (Jumanne, Desemba 28, 2021) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Lindi waliofika kumpokea kwenye uwanja wa ndege wa Nachingwea, mkoani humo.

 

Waziri Mkuu alisema ujenzi wa madarasa unaoendelea kote nchini hivi sasa, unalenga kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anakwenda shule iwe ni ya msingi au ni ya sekondari. “Tunataka tuondoe kabisa tabia ya kukuta watoto wetu wakifanya biashara kwenye stendi za mabasi au nyumba za starehe.”

 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wawahimize wananchi watunze akiba ya chakula walichonacho kwa sababu mkoa wa Lindi ni miongoni mwa mikoa ambayo bado haijaanza kupata mvua za vuli.

 

“Lindi ni miongoni mwa mikoa ambayo haijapata mvua hadi sasa. Lazima tujipange, tuangalie kwani yako mazao ya kibiashara na yako pia mazao ya chakula ambayo yanatumika kibiashara. Tutunze akiba tuliyonayo, tusitumie akiba hii kutengeneza pombe au kufanyia sherehe,” alisema na kuwasisitiza viongozi hao wakatoe elimu kwa wananchi.

 

Mapema, Mkuu wa Mkoa Lindi, Bibi Zainab Tellack alisema mkoa huo umekamilisha mauzo ya korosho isipokuwa kwa maeneo machache sana na wamefanikiwa kuuza tani milioni 63 zenye thamani ya sh. bilioni 131.

 

Kutokana na taarifa hiyo, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa mkoa na wilaya wabebe jukumu ya kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuwekeza kwenye miradi mbalimbali badala ya kutumia fedha hizo kwa starehe.

 

“Hatuwezi kuwafundisha watu namna ya kutumia fedha yao, lakini tunao wajibu wa kuwaelimisha. Tutoe miongozo ili wafanye uwekezaji, wajenge nyumba bora za kuishi, wanunue vifaa ili watoto waende shule na wajali afya zao,” alisema.

 

Waziri Mkuu yuko jimboni kwake Ruangwa kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.

Share To:

Post A Comment: