Na John Walter-Kiteto


Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, inamshikilia Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngeju Kata ya Namelock wilayani humo, Bw. Michael Noah Seru, kwa tuhuma za kuuza ardhi.


Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kiteto, Venance Sangawe alisema alifikia uamuzi wa kumkamata na kumweka ndani  Mwenyekiti huyo Kwa tuhuma za kuuza ardhi  na kumchunguza  kisha atafikishwa mahakamani kwa tuhuma hizo ambapo alipokea fedha za watu nane.


"Nimemkamata Mwenyekiti, Michael Noah Seru, na kumweka ndani kwanza.., tunamchungunza Kwa tuhuma ya kupokea fedha za watu nane hapa Kiteto akidai anataka kuwauzia ardhi ya Kijiji Jambo ambalo ni kosa kisheria lakini pia hana ardhi na hana mamlaka ya kuuza ardhi" alisema Sangawe.


Alisema migogoro mingi ya Ardhi Kiteto inasababishwa na baadhi ya wenyeviti wa vijiji ambao wanauza ardhi hiyo na mara kadhaa madhara makubwa yamekuwa yakijitokeza kwa wananchi yakiwemo kugombana na hata maafa kama ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita.


Mbali na Mwenyekiti huyo alisema katika Ofisi yake kuna madai mengi yanahusu ardhi hivyo ameanza na Mwenyekiti huyo kisha ataendelea na wengine ambao wanajihusisha kuuza Ardhi katika maeneo yao.


Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mbaraka Al Haji Batenga, katika Kikao cha Ushauri cha Wilaya ya Kiteto DCC, aliwataka wananchi kuepuka matapeli wa ardhi na kutakiwa kutoa taarifa mapema kwenye vyombo vya sheria.


Alisema migogoro ya Ardhi Kiteto bado ipo na mingi inachangiwa na baadhi ya viongozi wa Serikali za vijiji ambao wanaitumia migogoro hiyo kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao


Amesema kamwe hatofumbia macho migogoro ya ardhi akidai sheria kali zitachukuliwa dhidi ya walanguzi wa Ardhi ambao wamekuwa na madhara makubwa kwa jamii isiyo na uelewa wa kutosha Juu ya Ardhi ardhi.

Share To:

Post A Comment: