Wakulima wa mkoa wa Rukwa wameshauriwa kulima mazao yanayostahimili ukame kutokana na mwenendo wa unyeshaji mvua mwaka huu si wa kuridhisha.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ametoa ushauri huo (22.12.2021) mjini Sumbawanga wakati akizungumza kwenye kikao cha kusimamia, kuratibu na kudhibiti mapato na matumizi ya serikali robo ya pili kilichohudhuriwa na wakurugenzi wa halmashauri zote.

“Mvua zimechelewa sana. Katika wilaya zetu tumeshuhudia kiwango kidogo cha mvua hadi sasa hivyo ni wakati muafaka wataalam wa kilimo wakaelimisha wakulima kupanda mazao yanayostahimili ukame “alisisitiza Mkirikiti.

Mkirikiti aliongeza kusema tayari serikali imechukua hatua kadhaa ikiwemo kugawa mbegu za soya na alizeti ili wakulima wazalishe mazao hayo ambayo haihitaji mvua nyingi na kuwa jitihada zaidi zinatakiwa ikiwemo kutumia kilimo cha umwagiliaji katika mabonde yaliyopo ili kuwa na uhakika wa mazao ya chakula.

Katika hatua nyingine Mkirikiti amewagiza wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo kukamilisha miradi ya ujenzi wa madarasa chini ya mpango wa Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 ili yatumike kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2022.

Kuhusu kuongeza mapato ya halmashauri, Mkirikiti amewataka wakurugenzi hao kujikita katika kubuni vyanzo vipya visivyo kuwa kero kwa wananchi ili miradi ya maendeleo itekelezeke.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Denis Bandisa akizungumza kwenye kikao hicho aliwakumbusha viongozi wa halmashauri kuendelea kutenga fedha na kutekeleza afua za lishe ili kuondokana na tatizo la udumavu na utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano.

Mwisho.

Imeandaliwa na;

Afisa Habari Mkuu,

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa,

SUMBAWANGA

22.12.2021

Share To:

Post A Comment: