Ndugu Wananchi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekuwa ikitoa taarifa kwa wananchi kuhusiana na mwenendo wa magonjwa mbalimbali yakiwemo yale ya milipuko. Taarifa hii imekuwa ikienda sambamba na taarifa ya hatua zinazostahili kuchukuliwa kwa ajili ya kudhibiti magonjwa hayoAidha, wote tumeshuhudia Dunia ikipambana na mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19 ambapo, nchi mbalimbali zimeendelea kuchukua hatua za kukabiliana. Hata hivyo, kumekuwa na wimbi la pili na la tatu la mlipuko wa ugonjwa huo, ambapo nchi nyingi zimeathiriwa ikiwemo Tanzania. Aidha, hivi karibuni kumekuwa na tishio la wimbi la nne baada ya taarifa kutoka nchi mbalimbali Duniani.

Ndugu Wananchi, hadi kufikia tarehe 29 Novemba, 2021 jumla ya waliothibitika kuwa na maambukizi Duniani ni 260,867,011 na vifo 5,200,267 vimetolewa taarifa. Aidha, tangu kuripotiwa kwa ugonjwa huu hapa nchini Tanzania mnamo tarehe 16 Machi, 2020 hadi 28 Novemba 2021 jumla ya waliothibitika kuwa na maambukizi ni 26,273 na vifo 731 vimetolewa taarifa. Kwa ujumla baadhi ya nchi Duniani zikiwemo za Afrika zimeanza kuripoti ongezeko la visa vipya vya UVIKO 19 na hivyo kuleta tishio la kukumbwa na wimbi la nne la maambukizi ya ugonjwa huo.  

Kwa upande mwingine, hivi karibuni baadhi ya nchi zimeripoti ugunduzi wa anuwai mpya ya kirusi anayetambulika kwa jina la Omicron (B.1.1.529). Kama nchi hatuna budi kuendelea kuchukua hatua sahihi za kujikinga. Kwa msingi huu, tunahitaji kuongeza kasi zaidi ya kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO-19.

Ndugu Wananchi, jukumu la kinga dhidi ya magonjwa yote ni la kila mmoja wetu. Serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau wake imekuwa ikisimamia utekelezaji wa afua mbalimbali za kuwezesha jamii kujikinga na UVIKO-19. Aidha, Serikali imeendelea kuwezesha upatikanaji wa chanjo nchini ambapo hadi sasa imeshapokea jumla ya dozi za chanjo 4,305,750 ambazo zinatosha kuchanja wananchi 2,766,575. 

Aina ya chanjo zilizopokelewa mpaka sasa ni Jansen (J&J) dozi 1,227,400 ambapo mtu mmoja anachoma dozi moja, Sinopharm dozi 2,578,400 zitakazochanja watu 1,289,200 ambapo mtu mmoja anachoma dozi 2, na chanjo aina ya Pfizer dozi 499.950 zitakazochanja watu 249,975 ambapo mtu mmoja anachoma dozi 2.  

Ndugu Wananchi, Mpaka kufikia tarehe 28 Novemba 2021, jumla ya Wananchi waliopata chanjo ni 1,520,275 sawa na 2.7% ya watanzania wote. Kati ya hao, watanzania waliomaliza chanjo ni 1,027,818. Lengo la Serikali ni kufikia 60% ya watanzania wote waliopata chanjo dhidi ya UVIKO 19 hivyo wizara na wadau wake wote wataendelea kuelimisha na kutoa huduma ya chanjo. Aidha, natoa wito kwa kila aliyechanja amwelimishwe mwingine aone umuhimu wa kuchanja. 

Ndugu Wananchi, pamoja na juhudi hizi za uchanjaji, Serikali imeendelea na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ugonjwa huu nchini kwa kuendelea kuimarisha huduma za tiba. Mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza wigo wa upimaji wa UVIKO-19 nchini ambapo kwa sasa jumla ya Maabara 5 zilizopo Mikoa ya Dar es Salaam (Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii), Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Arusha na Dodoma pamoja na maabara katika Hospitali ya Bugando - Mwanza zinafanya upimaji wa virusi vya ugonjwa huu. Aidha, upimaji katika maeneo mengine utafuata ambapo kwa sasa mpango ni kuwezesha upimaji katika Hospitali zote za Rufaa za Mikoa.  

Ndugu Wananchi, pamoja na jitihada hizi, hatuna budi kuchukua tahadhari juu ya wimbi la nne la ugonjwa wa UVIKO-19. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaimarisha mikakakati ya kukabiliana na tishio hili ikiwemo kuwakumbusha wananchi kuzingatia miongozo ya kukabiliana na UVIKO-19 ambayo ni pamoja uvaaji wa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au vipukusi, kuzingatia kufanya mazoezi, mlo kamili na kutumia tiba asili kama inavyoelimishwa na wataalamu wa baraza la tiba asili.

Vilevile, kuendelea kuishirikisha jamii katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa huu nchini kwa kuendelea kutoa taarifa za ugonjwa huu kutoka maeneo mbalimbali duniani na ndani ya nchi, kutoa taarifa za viashiria vya mwenendo wa ugonjwa nchini na taarifa zingine zote ambazo zinaweza kuwa na msaada kwenye kupambana na ugonjwa huu. Kwa upande mwingine, kuimarisha uchunguzi katika viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu na kufanya ufuatiliaji wa nchi zenye ongezeko la wagonjwa na kuchukua hatua stahiki.  

Ndugu Wananchi, napenda kutoa rai kwenu kuwa twendeni tukachanje chanjo ya UVIKO-19. Chanjo hizi zinatolewa bure na kwa hiari na pia zimethibitishwa kuwa ni bora na salama na tayari nchini Tanzania watu wengi wameshapata chanjo hizi na wanaendelea na shughuli zao kwa kujiamini. Nichukue fursa hii kuwapongeza watanzania wanaoendelea kujitokeza kupata chanjo hizi katika vituo vyetu vya huduma za afya na vituo maalumu vya huduma za mkoba karibu na jamii.  

Kipekee nitambue mikoa 10 ambayo ilifanya kazi nzuri sana kipindi cha utoaji wa chanjo ya J & J ambayo ni Mtwara, Ruvuma, Kilimanjaro, Lindi, Mbeya, Dar es Salaam, Arusha, Pwani, Dodoma na Kigoma. Aidha, nipongeze pia Mikoa inayoenda kwa kasi zaidi sasa katika kutoa chanjo ya Sinopharm, ambayo ni Mwanza, Dodoma, Ruvuma, Kagera, Mara, Morogoro, Mbeya, Arusha, Lindi na Dar es Salaam.  Nitoe wito kwa Viongozi ngazi ya Mikoa na Halmashauri kuendelea kusimamia utoaji wa chanjo katika maeneo yao ili kuwafikia wananchi wengi zaidi. Niwakumbushe wale waliopata chanjo moja ya Sinopharm kurudi kuchanja dose ya pili ili wapate kinga kamili.

Ndugu Wananchi, nawaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Waganga Wafawidhi wa Hospitali zote nchini pamoja na Timu zote za Usimamizi wa Afya za Mikoa na Halmashaurikuendelea kufanya ufuatiliaji na kutuma taarifa za wagonjwa kwa miongozo na maelekezo waliyopewa na Wizara. Na kwa watoa huduma za Afya wote nchini nasisitiza yafuatayo:

1.    Kuimarisha upokeaji wa taarifa kutoka kwenye jamii kupitia Madawati ya kufuatilia Tetesi “Alert Desk”.

2.    Wahisiwa wote wa ugonjwa wa UVIKO-19 watolewe sampuli kuongeza wigo wa upimaji, ili kujua mwenendo wa ugonjwa katika maeneo yetu.

3.    Hospitali zote za Taifa, Kanda, Mikoa na Wilaya, na vituo vya kutolea huduma za afya, ziimarishe mfumo wa kubaini wagonjwa mapema. 

4.    Watoa huduma kwenye vituo vya kutolea huduma waendelee kuzingatia Miongozo ya Matibabu na Miongozo ya Kuzuia maambukizi. 

Ndugu Wananchi, Nipende kuwasihi kutokuwa na hofu bali tuendelee kuwa watulivu na kutekeleza shughuli za maendeleo huku tukichukua tahadhari zote. Aidha, Wizara inaendelea kupokea taarifa na viashiria vya magonjwa yote ya milipuko kutoka kwa wananchi zikiwemo za UVIKO-19 kupitia namba ya simu 199 bila malipo yoyote. Wizara itaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa magonjwa ya milipuko nchini kila baada ya siku kumi hivyo mara tatu kwa mwezi. Mwisho, wananchi zingatieni matamko na taarifa kutoka vyanzo rasmi, epukeni vyanzo visivyo rasmi. 


Share To:

Post A Comment: