Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella ametangaza rasmi zoezi la kuanza kuwahamisha machinga kuanza Novemba 1,2021 hadi Novemba 3,2021 Jijini Arusha.


Ameyasema hayo alipokuwa akikagua ujenzi wa masoko hayo yaliyopo Engutoto Njiro, soko la Mbauda,eneo la Machame Luxury, eneo la Ulezi na kiwanja namba 68 Kilombero.


"Zoezi la kuwapeleka machinga katika maeneo yao ya masoko mapya katika Jiji la Arusha litakuwa la utulivu na utaratibu unaoeleweka",alisema.


Aidha, amesema kinachotakiwa ni ushirikiano kwa watu wote na zoezi litakuwa rahisi na la amani.


Mongella amesema katika hali ya kuliweka Jiji la Arusha nadhifu na la kuvutia wamachinga hao watapangwa kulingana na aina ya bidhaa wanazouza. 


Amesema Soko la Engutoto litakuwa maalumu kwa bidhaa za thamani tu na wahusika ndio watajenga wenyewe mabanda yao.


Alikadharika soko la Mbauda litakuwa la nguo za mitumba, soko la Machame litakuwa la vyombo na vifaa vya umeme, soko la Ulezi litakuwa maalumu kwa nguo za dukani na soko la Kilombero kiwanja namba 68 litauza mbogamboga na Matunda tu.


Mongella amewataka wamachinga wote kutumia hizo siku 3 alizotoa kuhamia katika masoko hayo kwa utaratibu utakaokuwa unatangazwa na magari ya Serikali.


Pia, amewataka wafanyabiashara wa maduka kurudisha bidhaa zao ndani ya maduka kwani baadhi yao walitoa nje ya maduka ili kutafuta wateja kupitia kwa machinga hao.


Vile vile amewataka wafanyabiashara katika soko ya Kilombero na soko Kuu kuhakikisha wanakaa kwenye meza zao na kulipa kodi  kulingana na makubaliano yaliyopo na Halmashauri ya Jiji la Arusha.


Ametahazalisha kwa watakaoshindwa kurudi katika maduka na meza zao katika masoko hayo basi watapewa wafanyabiashara wengine waliokosa maeneo.


Amesema faida kubwa ya kuwapanga wamachinga ni kuliweka Jiji katika mpangilio unaovutia kwani ni mji wa kitalii lakini pia utasaidia wamachinga kutambulika na Serikali kwa urahisi na hivyo kuwa na fursa rahisi ya kupewa mikopo ya Halmashauri.


Nae, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt. John Pima amewataka wafanyabiashara wote waliokimbia vibanda na meza zao katika masoko kufikia Novemba 1,2021 wawe wamerudi katika maeneo yao na ukaguzi utafanyika siku hiyo.


Amesema kila machinga atakaepewa kibanda atapewa kitambulisha cha machinga cha Jiji ili watambulika kirahisi.


Mwenyekiti wa wamachinga Mkoa wa Arusha Bi. Amina Njoka amewataka wamachinga wote watulie wakisubiri maelekezo ya namna zoezi hilo la kuwapanga katika maeneno yao litakavyofanyika.


Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wamachinga hao na kuwawekea  utaratibu mzuri wa ufanyaji biashara utakaowafanya watambulike na kunufaika nao.


Zoezi hilo la kuwapanga machinga limetangazwa rasmi kuanza Novemba 1 hadi Novemba 3 ikiwa ni maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan Septemba 13, 2021 na kusisitizwa zaidi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mnamo septemba 15, 2021.

Share To:

Post A Comment: