Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka watendaji wa sekta ya maji nchini kuhakikisha wanazingatia vigezo wakati wa utekelezaji wa miradi ya maji kupitia fedha zilizotolewa na serikali ikiwa ni Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO -19.


Amesema Mheshimiwa Rais Samia ameelekeza shilingi Bilioni 139.4 kwa Wizara ya Maji kwa lengo la kuhakikisha zinatumika kuondoa changamoto ya maji, hivyo lazima watendaji wazingatie maelekezo na weledi wao katika kufanikisha azma ya Serikali.


“Mheshiwa Rais amepambana hadi kupata mkopo wa shilingi trilioni 1.3 kama mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na ameelekeza shilingi Bilioni 139.4 ziletwe Wizara ya Maji. Hii ni imani kubwa na mapenzi mazito ya Rais kwa Watanzania ambao bado wanahitaji tuwafikie  kupata huduma ya maji. Ukiaminiwa, aminika. Mheshimiwa Rais ametuamini, lazima tumuonesha kwamba tunaweza.”  Waziri Aweso amesema.


Amefafanua matumizi ya fedha hizo kuwa Bilioni 104.2 zimepangwa kutekeleza miradi 218. Bililioni 17.5 kununua seti 25 za mitambo ya kuchimba visima. Bilioni 17.6 kununua seti 5 za mitambo ya ujenzi wa mabwawa pamoja na seti 4 vifaa vya utafiti wa maji.


Naye Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amesema jitihada kubwa imefanyika kuhakikisha huduma ya maji inawafikia Watanzania wengi lakini bado watendaji wanapaswa kuhakikisha wanatekeleza maagizo ya viongozi ili thamani ya fedha ionekane katika miradi inayotekelezwa. 


Pia amewataka kuhakikisha wanawashirikisha na kuwapa taarifa viongozi wa serikali na wawakilishi wa wananchi walioko katika maeneo ambayo miradi hiyo inatekelezwa. 


Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma Mheshimiwa Waziri Aweso   ametoa tuzo kwa maabara saba za Ubora wa Maji hapa nchini ambazo zimefanikiwa kupata Ithibati. Kwa kiwango hicho,  Maabara hizo sasa zinaweza kufanya kazi ya kuangalia ubora wa maji mahali popote Duniani, baada ya kukidhi vigezo vyote vya kimataifa.

Share To:

Post A Comment: