Katibu wa Idara ya Seneti Vyuo na Vyuo Vikuu ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida Paulo Dotto akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tawi jipya la UVCCM ndani ya Chuo cha Ualimu Kinampanda, kilichopo Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Matukio ya hafla ya uzinduzi yakiendelea.
Mamia ya wanachuo wa Chuo cha Ualimu Kinampanda wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi huo wa Tawi jipya la UVCCM chuoni hapo.
Muadili wa chuo hicho Mwalimu Nestory Sikalengo (aliyesimama kulia) akizungumza kwenye hafla hiyo.Makamu Mkuu wa Chuo cha Ualimu Kinampanda Gimenye Gesimba Motiba  (aliyesimama kulia) akishiriki kikamilifu katika uzinduzi huo.
Rais Mstaafu wa chuo hicho Paul Renatus akieleza faida za mwanachuo na kijana wa Tanzania kujiunga na Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM)
Makamu Mkuu wa chuo hicho Gimenye Motiba akiongoza viongozi na baadhi ya wajumbe wa UVCCM kuangalia ukarabati mkubwa wa miundombinu uliofanywa na serikali ndani ya chuo hicho.
Katibu wa Seneti Paulo Dotto (katikati) akiongoza wajumbe na viongozi wa UVCCM kuelekea kwenye hafla ya uzinduzi huo.

Baadhi ya viongozi wa UVCCM walioshiriki kwenye hafla hiyo. Kutoka kulia Afisa wa CCM Wilaya ya Singida Omary Mwangi, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Singida Mjini Seleman Dafi, Katibu wa Seneti Vyuo na Vyuo Vikuu Paulo Dotto, Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Mwankoko Singida (Kamanda) Tumaini Jackson, Mjumbe wa UVCCM Paul Renatus, Kaimu Katibu wa Hamasa Mkoa Daniel Kisinza na Mjumbe Seneti Mkoa Almachius Ibrahim

Viongozi wapya wakiwa na baadhi ya wajumbe wa Seneti.
Afisa wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Singida Mjini Omary Mwangi akizungumza na baadhi ya wajumbe kabla ya kuanza hafla ya uzinduzi wa Tawi hilo.
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Singida Mjini Seleman Dafi akizungumza kwenye hafla hiyo.
Baadhi ya viongozi wa Seneti wakipokewa na uongozi wa chuo hicho  baada ya kuwasili chuoni hapo.

Wimbo wa chama ukiimbwa.
Wanachuo wa Chuo cha Ualimu Kinampanda wakipiga kura kuchagua viongozi wa Tawi hilo jipya la UVCCM.


Na Godwin Myovela, Singida.


SENETI ya Vyuo na Vyuo Vikuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida hatimaye imezindua Tawi jipya la Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) ndani ya chuo kikongwe cha Ualimu cha Kinampanda, kilichopo Wilaya ya Iramba mkoani hapa.

Sherehe za uzinduzi huo ambazo zilikwenda sambamba na kampeni za kuvutia zilizolenga kuwapata viongozi wa seneti wa Tawi hilo kwa mara ya kwanza tangu kuanzisha kwa chuo hicho mwaka 1975 ziliibua shangwe na hamasa kubwa kwa idadi ya mamia ya wanachuo waliohudhuria tukio hilo la kihistoria.

Akizungumza wakati akiongoza hafla ya uzinduzi huo, Katibu wa Seneti Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Singida, Paulo Dotto kwa niaba ya UVCCM mkoa, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoonesha hali ya upendo na kuwajali vijana wa chuo cha Kinampanda kwa namna serikali yake ilivyotumia zaidi ya Shilingi Bilioni Moja kwa kufanya ukarabati mkubwa wa miundombinu ya chuo hicho.


Aidha, Dotto alishukuru hatua ya serikali chini ya Rais kwa kubeba dhamana ya kulipa gharama zote za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa mwaka wa pili wa chuo hicho, ikiwemo vifaa na posho kwa mfululizo wa siku zote 60 za kipindi cha mafunzo yao kwa vitendo jambo lililoibua hamasa, faraja na kuchagiza ari ya vijana chuoni hapo kuendelea kukiamini na kukipenda Chama Cha Mapinduzi.

Kuhusu hatua ya kushusha tozo za miamala kwenye simu za viganjani Katibu huyo wa Seneti kwa niaba ya vijana alipongeza usikivu wa hali ya juu wa CCM ambayo ndio inasimamia serikali kwa namna ilivyoonyesha kuthamini, kujali na kuchukua hatua juu ya mawazo yaliyowasilishwa na wananchi kwa hatua zaidi za utekelezaji.

"Mambo yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika ni mengi sana, tunaamini nia na dhamira ya serikali kwa vijana ni njema sana. Tuzidi kukiunga mkono chama chetu kwa tija na ustawi uliopo wa usambazaji wa huduma zake unaoendelea kwa kasi ndani ya jamii," alisema Dotto.

Hata hivyo alishauri vijana kutumia fursa mbalimbali zilizopo ikiwemo kutumia kikamilifu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa mahususi kwa makundi ya vijana, wanawake na wenye ulemavu kwa kujishughulisha na ujasiriamali ambao ni matokeo ya mafunzo na taaluma mbalimbali wanazopatiwa vijana wakiwa vyuoni.

Katika hatua nyingine, na kwa namna ya kipekee, Dotto kwa niaba ya Seneti mkoani hapa alimpongeza Rais Samia kwa namna alivyoamua kubeba jukumu kubwa la kutangaza vivutio vya Tanzania Kimataifa jambo alilobashiri kuwa ni kiashiria chanya ambacho kinakwenda kuleta mapinduzi makubwa ndani ya sekta ya utalii.

"Suala hili sio tu litaleta tija kubwa katika muktadha mzima wa ustawi kwenye sekta ya utalii bali litachagiza ongezeko la watalii na nchi kupata fedha za kigeni. Niwasihi vijana wenzangu wa vyuo na vyuo vikuu...hatma ya nchi ipo mikononi mwetu tuunge mkono ubunifu huu kwa kumtia moyo Mheshimiwa Rais," alisisitiza.

Katika hafla ya uzinduzi wa Tawi hilo, Asia Kalungula aliibuka mshindi na kutangazwa Mwenyekiti wa Tawi hilo jipya la UVCCM Chuo cha Ualimu Kinampanda, huku nafasi ya Katibu ikichukuliwa na Joseph Lubegeja na kura nyingine za kishindo zilimwangukia Ridhiwan Rashid kwa nafasi ya Katibu wa Hamasa.Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: