Na Mwandishi Wetu


Katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imewapandisha vyeo walimu 126,346 na kati yao walimu 121,663 sawa na asilimia 96.2 wabebadilishwa mishahara yao kutoka ile ya vyeo vya zamani kwenda katika vyeo vipya.Zoezi la kuwapandisha vyeo walimu linahusisha kwa karibu Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na Ofisi ya TSC katika Wilaya husika  ambapo mwajiri anawasilisha mapendekezo ya walimu wanaotakiwa kupandishwa, Katibu Msaidizi anafanya uchambuzi na kuwasilisha mapendekezo hayo kwenye Kamati ya TSC ngazi ya Wilaya kwa ajili ya Uamuzi na kisha Katibu Msaidizi anawaandikia walimu barua za kupanda cheo.  Kwa mujibu wa wadau mbalimbali wakiwemo walimu wenyewe, zoezi la upandishaji vyeo watumishi wa umma wakiwemo walimu lililofanyika miezi michache iliyopita lilitekelezwa kwa ufanisi mkubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.


Kauli hiyo inaungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia elimu, Gerald Mweli ambaye anaipongeza TSC kwa kusimamia zoezi hilo kwa weledi na kufanya aslimia 96 ya walimu waliopandishwa madaraja kubadilishiwa mishahara.


Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu huyo anaeleza kuwa pamoja na zoezi hilo kufanyika kwa ufanisi zipo changamoto zilizojitokeza ambapo baadhi ya watendaji wanalalamikiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kutoa upendeleo kwa baadhi ya walimu ambao hawakuwa na sifa za kupanda vyeo huku wenye sifa wakiachwa.


Kutokana na changamoto hiyo, Naibu Katibu Mkuu Mweli ameiagiza Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), kufanya tathmini ya wazi katika zoezi la upandishaji vyeo walimu lililofanyika hivi karibuni ili kubaini kama kila mwalimu aliyestahili kupandishwa cheo amepata haki hiyo. 


Mweli ametoa agizo hilo Septemba 20, 2021 wakati akifungua mafunzo ya siku mbili yaliyowakutanisha wajumbe wa Kamati za TSC ngazi ya Wilaya kutoka katika Wilaya za Mikoa ya Dodoma, Singida, Iringa na Manyara yanayofanyaika kwa siku mbili katika Chuo cha Mipngo, Dodoma. 


Kiongozi huyo ameeleza kuwa yapo malalamiko kuwa baadhi ya watumishi wasio wa adilifu walitumia vibaya mamlaka waliyonayo katika kupandisha vyeo walimu na kujihusisha na vitendo vya rushwa kitu ambacho kimesababisha baadhi ya walimu kukosa haki yao ya kupandishwa madaraja.


“Natambua kazi kubwa ambayo inafanywa na TSC hasa katika zoezi la kupandisha madaraja walimu. Lakini pamoja na kazi hiyo zipo changamoto ambazo tumeziona wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo. Wapo baadhi ya Kaimu Katibu Wasaidizi ambao wanatuhumiwa kwa rushwa. Ninahitji mfanye tathnini katika Wilaya zote muone namna zoezi hilo lilivyokwenda,” aliesema Mweli.


Alisisitiza kuwa anataka tathmini hiyo iwe na vigezo vya wazi ili kuona kama kila mwalimu aliyekuwa na sifa za kupanda daraja amepandishwa na kama kuna ambao hawakuwa na sifa lakini wamepandishwa ili hatua stahiki zichukuliwe kwa watumishi wote waliokiuka utaratibu uliotolewa.


“Hapa ukitaka kufuatilia suala la rushwa inaweza ikawa ngumu kuthibitisha moja kwa moja lakini tukiweka vigezo vya wazi tutapata majibu. Kama utakuta mwalimu hana sifa lakini kapandishwa na mwenye sifa hajapandishwa, ni wazi kuwa kuna mchezo umefanyika na lazima tuchukue hatua”, alisisitiza Naibu Katibu Mkuu.


Ameeleza kuwa kunapokuwa na baadhi ya watendaji ambao sio waadilifu, sio tu kwamba wanawakosesha walimu haki zao bali pia inachafua taswira ya Tume ya Utumishi wa Walimu na kusababisha chombo hicho kukosa heshima na kutoaminiwa na jamii.


“Anapotokea mtumishi mmoja kati yenu akajihusisha na rushwa matokeo yake ni kwamba TSC yote inaonekana kuwa ni ya wala rushwa. Hivyo Katibu wa Tume, hili naomba tulikemee kwa nguvu zote ili walimu waweze kuhudumiwa kwa haki kwa kuzingatia sheria,” alieleza Mweli.


Akizungumzia kuhusu mafunzo hayo, Mweli alisema kuwa Kamati za Wilaya zinaundwa na wajumbe wenye taaluma tofauti tofauti na wanatakiwa kushughulika na masuala ya utumishi wa walimu, hivyo ni muhimu wapatiwe mafunzo ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Niwapongeze sana TSC kwa kuona umuhimu wa kufanya mafunzo haya kwa kuwa hizi kamati za wilaya ndizo hasa zinazotekeleza majukumu ya msingi ya Tume. Hivyo ili waweze kufikia matarajio mnayoyataka ni lazima muwajengee uwezo wa namna ya kufikia malengo hayo. Baada ya mafunzo haya watakapoboronga mna haki ya kuwauliza kwa kuwa tayari mmewawezesha,” alieleza.


Naye Mwenyekiti wa TSC, Willy Komba alisema kuwa TAMISEMI imekuwa na ushirikiano wa karibu sana na TSC na hivyo imeisaidia Tume hiyo kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinaikabili hususan katika ofisi zake za wilayani.


“Ndugu Naibu Katibu Mkuu sisi tunakushukuru wewe binafsi pamoja na ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ushirikiano mkubwa ambao tunaupata kutoka kwenu. Mmesaidia watumishi wetu wetu wa wilayani kupata ofisi kwa Wakurugenzi na mmekuwa mkitusaidia kwenye masuala ya miundombinu mbalimbali. Tunawashukuru sana na tunaomba ushirikiano huu uendelee kuwepo wakati wote,” alisema Prof. Komba.


Kwa uapande wake, Katibu wa TSC, Paulina Nkwama alitumia mkutano huo kukemea vitendo vya rushwa kwa watumishi wa Tume hiyo huku akieleza kuwa hatamvumilia yeyote atakayejihusisha na vitendo hivyo ambavyo  vinaleta aibu kwa Taasisi anayoiongoza.


“Naomba kila mtumishi azingatie maadili ya kazi. Naibu Katibu Mkuu amezungumzia uwepo wa malalamiko ya wateja kuhusu baadhi ya watumishi. Mimi nitashirikiana na kila mtumishi anayefanya kazi yake kwa kuzingatia maadili ya kazi, lakini kwa yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo vya rushwa nitakuwa mstari wa mbele kumchukulia hatua,” alisema Nkwama.


Awali, akitoa maelezo ya utangulizi, Katibu huyo alieleza kuwa TSC imeweka utaratibu wa kutoa mafunzo kwa Kamati za Wilaya ili ziweze kutambua na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kutoka huduma bora kwa walimu.


Alifafanua kuwa moja ya majukumu ya Kamati za Wilaya ni kushughulikia mashauri ya nidhamu kwa walimu ambayo uendeleshaji wake unahitaji uelewa wa Sheria na Kanuni za TSC na za Utumishi wa Umma, hivyo ni muhimu kutoa mafunzo hayo  ili waweze kutenda haki wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

“Tumetoa mafunzo haya kwenye kanda mbili, hii ni ya tatu, tumefikia Mikoa 12 na tumebakiwa na Mikoa 14. Mafunzo haya yamekuwa na faida sana katika utekelezaji wa majukumu ya Kamati. Hata ukiangalia kwenye uendeshaji wa mashauri ya nidhamu, kumekuwa na mabadiliko makubwa ikilinganishwa na siku za nyuma,” alisema Nkwama.


Katika mafunzo hayo mada mbalimbali zinatarajia kutolewa ikiwa ni pamoja na; majukumu ya TSC kuhusu Ajira na Maendeleo ya Walimu, Maadili ya kazi ya ualimu, Mamlaka za Nidhamu na Rufaa kwa Walimu na majukumu yake, Taratibu za uendeshaji wa vikao vya Kamati za Wilaya, Muundo wa TSC pamoja na Historia ya TSC.

Share To:

Post A Comment: