Wafadhili wa Taasisi ya Kiislamu Al-Swadiq Al-Ameen wameunga mkono jitihada za Serikali na kujenga jengo la kutoa huduma ya mama na mtoto zahanati ya Bisheke iliyopo kata ya Bisheke lililogharimu kiasi cha Tsh. Milioni 37.


Akizindua jengo hilo Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila ameishukuru taasisi hiyo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwao na wadau wote wa maendeleo wanaojitoa kuleta maendeleo wilayani Muleba.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mhe. Nguvila amempongeza Sheikh Maulana Ramadhani Kawaga kwa kuona uhitaji wa jengo hilo na kuamua kuja kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kazi nzuri ya kuwajengea wana Bisheke jengo la mama na watoto litakalotumika kwa ajili ya huduma za uzazi.


"Kazi mnayoifanya ni nzuri sana, gharama mliyoitumia hapa mngeweza kwenda kuitumia kwa matumizi yenu mengine ila kutokana na utume uliopo ndani ya mioyo yenu mkaona mje kuwekeza katika huduma hii. Kama msingekuwa na utume huu msingeweza kufanya hii kazi kwa sababu hiyo fedha mngeamua kuitumia na familia zenu hakuna ambaye angewauliza. Lakini Mwenyezi Mungu amewaelekeza kuuleta huu msaada Bisheke kwenye wilaya yetu ya Muleba. Nawashukuru sana na ninawapongeza sana." Ameeleza Mhe. Toba Nguvila.


Aidha, Mhe. Nguvila ameeleza kuwa kwa msaada huu wa jengo la mama na mtoto akina mama wajawazito watakapokuwa wakijifungua salama wataendelea kuwaombea wafadhili. Amezitaja baadhi ya faida za jengo la huduma ya mama na mtoto kuwa linakwenda kuokoa maisha ya akina mama wajawazito, kuondoa vifo vya mama na watoto wakati wa kujifungua na kumsaidia mama kujifungua katika mazingira bora na salama.


Baada ya kukagua ujenzi wa jengo hilo Mhe. Nguvila ameridhishwa na ujenzi wa jengo hilo na kueleza kuwa ubora wa jengo hilo umezingatiwa na thamani ya fedha iliyotolewa imeonekana huku akiahidi kuwaletea umeme badala ya kuendelea kutumia nishati ya umeme jua (solar) kwa kumuagiza Meneja wa TANESCO kwenda kupima eneo hilo mpaka nguzo zinapoishia ili kuweza kutatua changamoto ya umeme utakaoboresha utoaji wa huduma bora.


"Nafahamu hapa kuna changamoto ya umeme, hii nishati ya umeme wa jua haiwezi kutumika kwa baadhi ya vifaa hususani vinavyotumika kwa akina mama wakati wa kujifungua zipo mashine zinazohitaji umeme mwingi, namuagiza Meneja wa TANESCO aje apime hapa na kuona idadi ya nguzo zinazohitajika kuanzia zilipoishia halafu tuone utaratibu wa namna ya kufikisha umeme kwenye zahanati hii." Amehaidi Mhe. Nguvila.


Kwa upande wake mwakilishi wa Kanda wa Taasisi ya Al Swadiq Al Ameen Sheikh Maulana AbdulMalik Kawaya ameeleza kuwa chanzo cha kujengwa kwa jengo la huduma ya mama na mtoto ni pale mdhamini mkuu wa jengo hilo alipokutana na mama anajifungua njiani kisha  akamueleza Sheikh Maulana kwamba hata mama yake kipindi anamzaa yeye alipoteza uhai wake, ndipo mdhamini huyo aliamua kujitolea kujenga jengo hilo la mama na mtoto na kutoa taarifa kwa Diwani. 

Baada ya hapo alioneshwa eneo  na fedha ikatolewa ujenzi ukaanza.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba Mhe. Magongo Justus amesema kuwa kutokana na ujenzi huu ni wakati sasa wa kata ya Bisheke kuwekwa katika mpango wa Halmashauri ili kuwa na kituo cha afya.


Pamoja na uzinduzi huo Mhe. Nguvila ameshauri kuwa ni vema uongozi wa kata ya Bisheke ukaona haja ya kuwa na benki ya matofali itakayowawezesha kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo. 


"Mnapokuwa na benki ya matofali hata mkipanga kujenga Kituo cha Afya inakuwa ni rahisi sana, ni rahisi hata kwa Mwenyekiti kumueleza Mkurugenzi kwa kuwa katika zahanati ya Bisheke kuna uhitaji wa bati kadhaa kwa ajili ya kuezeka majengo ya kituo cha Afya na Mkurigenzi kutekeleza jukumu hilo" ameleza Mhe. Mkuu wa wilaya.


Diwani wa kata ya Bisheke Mhe. Alexander Petro kwa niaba ya wananchi wa kata ya Bisheke ametoa shukrani kwa wafadhili kwa kuona uhitaji wao na kuwajengea jengo hilo ambalo litawasaidia sana akina mama na watoto na jamii ya watu wa kata ya Bisheke kwa ujumla.


Imetolewa na:


Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,

Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.

Share To:

Post A Comment: