Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila amekemea vikali vitendo vya uharibifu unaofanyika katika misitu ya asili iliyopo wilayani Muleba na kuonyesha kutoridhishwa na hali iliyopo sasa ya uhifadhi wa msitu wa Ruiga uliopo kata ya Kyebitembe na kata ya Kimwani baada ya kutembelea na kukagua hifadhi ya msitu huo.


Akizungumza baada ya kukagua msitu huo Mhe. Toba Nguvila, amesisitiza viongozi pamoja na jamii kwa pamoja kushirikiana kutunza rasilimali za msitu huo ili uwe endelevu kwa manufaa ya vizazi hadi vizazi. 


"Kuna wajibu wa TFS kama walengwa na wasimamizi wakuu wa uhifadhi wa misitu na kuna jamii ambao ndio wanufaika wa moja kwa moja na hii misitu iliyoko hapa, hivyo kwa pamoja tunatakiwa kushiriki kwa kiwango kikubwa katika uhifadhi wa msitu huu. Tunapokuwa na watoa taarifa wa kutosha pamoja na doria za mara kwa mara tutafanikiwa kudhibiti uharifu unaofanyika katika hifadhi hii. Hivyo naagiza kuboresha mbinu za watoa taarifa juu ya watu wanaofanya vitendo vya uharifu vitakavyoendelea kutokea katika eneo hili ili kuweza kukabiliana na majangili wanaoharibu rasilimali za hifadhi hii, sambamba na TFS kubadilisha na kuboresha mbinu za kupambana na wahalifu" ameeleza Mhe. Toba Nguvila.


Wakati wa ziara hiyo Mhe. Mkuu wa wilaya na wajumbe wa Kamati ya Usalama wameonesha kutoridhiswa na hali ya uhifadhi wa msitu hasa baada ya kukuta baadhi ya maeneo katika hifadhi hiyo yamechomwa moto na miti imekatwa. Aidha, kwa vitendo vya kijangili vilivyobainika ndani ya hifadhi hiyo Mhe. Nguvila amesisitiza mashimo yaliyokutwa kwenye hifadhi yafukiwe, ipandwe miti ya asili kwa ajili ya kutunza uoto wa asili pamoja na kutoa mwanya kwa watu kufanya shughuli za ufugaji nyuki zitakazosaidia kama sehemu ya ulinzi na kuongeza uchumi kwa wananchi.


"Nimetembea na kuona sehemu kubwa ya msitu huu imeharibiwa, majangili wanavamia na kukata miti, mifugo inaingizwa ovyo na uchomaji ovyo wa moto. Ni lazima tupande miti ya asili ya kutosha kutunza uoto wa msitu huu, tutoe mwanya kwa watu kufuga nyuki kuweka mizinga ya nyuki hata msitu mzima kwa sababu nyuki zitasaidia katika ulinzi, kukuza uchumi wa wananchi  na kutumika kama dawa kwa sababu unapokuwa na asali pamoja nyuki ni dawa. Baada ya wiki mbili nitarudi na wajumbe wa kamati ya Usalama kukagua kama maelekezo haya yamefanyiwa kazi," aliendelea kueleza Mhe. Nguvila.


Hata Hivyo, Mhe Toba Nguvila amewasisitiza viongozi wakiwemo maafisa Tarafa, Watendaji na Wenyekiti kufanya mikutano ya kuelimisha na kutoa maonyo na makatazo mbalimbali ili waachane na vitendo vya uharibifu wa pori kwa njia watu kuvuna miti hovyo pamoja na kuingiza mifugo ndani ya hifadhi ya pori hilo. Aidha alisisitiza pamoja na makatazo hayo ni vema wananchi wakaelezwa sheria ilivyo ikiwa ni pamoja na adhabu zake pindi zinapokiukwa.


Kwa upande wake Meneja wa wakala wa Misitu (TFS) wilaya ya Muleba, Bw. Mashaka Mrisho ameeleza kuwa amepokea maelekezo na maoni yote yaliyotolewa na anakwenda kubadili mbinu za ulinzi shirikishi kwa kuwa na ushirikiano wa pamoja kwa ajili ya kukabiliana na majangili wanaofanya uharibifu ikiwa ni pamoja na kuongeza kufanya doria za mara kwa mara sambamba na ukaguzi wa mara kwa mara ili kuendelea kuboresha pale ambapo kuna mapungufu.


Imetolewa na:


Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,

Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.

Share To:

Post A Comment: