Baadhi ya Viongozi wa PURA wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa CHAVITA Lindi mara baada ya kumalizika kwa mafunzo.

********************************

Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Mkoani Lindi kimeishukuru Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA) kwa kuwapatia mafunzo kuhusu shughuli za utafutaji na uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi asilia nchini.

Mafunzo hayo yalitolewa hivi karibuni Wilayani Ruangwa – Lindi wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Kimataifa ya Viziwi Duniani (kwa ngazi ya Wilaya) ambapo PURA ilishiriki kama mmoja wa wafadhili wa maadhimisho hayo na mtoa mada.

Maadhimisho hayo yaliratibiwa na CHAVITA Lindi kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Watu Wenye Ulemavu na kuhusisha washiriki takribani 60 wenye changamoto za usikivu, kuona na ulemavu wa viungo.

Akifungua mafunzo hayo, Katibu Tawala Wilaya ya Ruangwa, Bw. Shaban Ismail Namanga ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa alisema PURA imefanya jambo la kipekee kwa kuwa kundi la watu wenye ulemavu ni kundi ambalo husahaulika aghalabu katika masuala ya mafuta na gesi asilia.

“Nipende kuwapongeza PURA kwa kutambua kundi hili na kuona umuhimu wa kuwapatia mafunzo. Hii ni ishara tosha kuwa mnatekeleza vyema majukumu yenu kwa kuzingatia usawa na kuhakiisha kuwa watanzania wote wanakuwa na uelewa wa masuala ya mafuta na gesi”, alieleza Bw. Shaban.

Katika maadhimisho hayo PURA iliwakilishwa na Mkuu wa Idara ya Masuala ya Ufundi (Mha. Danstan Asanga), Mkuu wa Kitengo cha Ushiriki wa Wazawa na Ushirikishwaji wa Wadau (Bw. Charles Nyangi), na Afisa kutoka Idara ya Masuala ya Ufundi (Bw. Faustine Matiku).

Wawakilishi hao waliwasilisha mada tatu zilizojikita katika maeneo ya historia ya utafutaji wa mafuta na gesi nchini; miongozo ya kisheria na kitaasisi katika sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini; na ushiriki wa Watanzania katika sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia.

Akiwasilisha mada kuhusu ushiriki wa watanzania, Bw. Nyangi alieleza kuwa PURA imejipanga vyema kuhakikisha kuwa ushiriki wa watanzania katika shughuli za mkondo wa juu petroli ni jumuishi na kwamba kundi la watu wenye ulemavu haliachwi nyuma.

Aidha, Bw. Nyangi alieleza kuwa kwa mujibu wa kifungu namba 12(2) cha Sheria ya Petroli, 2015; PURA inajukumu la kuhahikisha kuwa wadau/makundi mbalimbali yanapatiwa elimu kuhusu mkondo wa juu wa petroli na fursa zilizopo.

Katika neno la shukrani, Mwenyekiti wa CHAVITA – Lindi, Bw. Sultan Akbar aliishukuru PURA kwa kuwezesha na kushiriki katika maadhimisho ya siku yao.

“Hakika ushiriki wenu katika maadhimisho haya ni faraja kubwa na hakika tumejifunza mengi kuhusiana na masuala ya mafuta na gesi. Masuala ambayo mengi yalikuwa mageni kwetu. Vile vile tumefarijika kuona namna ambayo PURA inasimamia ushiriki wa watanzania wote bila kubagua ni kundi la walemavu ama la. Ni matumaini yetu kuwa zoezi hili litakuwa endelevu na mtazidi kufikia makundi mengi zaidi ya watu wenye ulemavu”, alihitimisha Bw Sultan.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: