Na John Walter-Babati

Wananchi wa Kata za Riroda na Ayasanda wilaya ya Babati mkoani Manyara wamempongeza mbunge wa Jimbo hilo Daniel Sillo kwa kuwatembelea na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao.

Wananchi hao wanasema awali hawakuwahi kumshuhudia mbunge akiwatembelea baada ya kuchaguliwa  hadi uchaguzi ulipokaribia hivyo alichofanya Sillo ni ishara kuwa yupo tayari kuwahudumia Kama alivyowahidi.

Wakizungumza katika mkutano wa mbunge wananchi hao wamesema kilio chao kikubwa ni miundo mbinu ya barabara,umeme kwa baadhi ya maeneo ya vijijini na vitongoji vyao.

Mheshimiwa Daniel Sillo alitembelea zahanati ya Endanachan Kata ya Ayasanda na kushuhudia ujenzi wa nyumba ya mganga ukiendelea ambapo umefikia hatua ya upauzi ikiwa ni nguvu za wananchi na serikali.

Aidha Sillo akiwa ameongozana na wataalamu kutoka Halmashauri ya wilaya ya Babati na viongozi wa chama cha Mapinduzi aliitembelea shule ya Msingi shikizi ya Ayatlaa iliyopo kata ya Riroda ambayo inasubiri fedha kwa ajili ya kumalizia madarasa mawili ambayo tayari yameezekwa bati.

Katika Mkutano huo uliofanyika Kijiji cha Endanachan na Riroda, maswali mengi yalihusu Umeme na barabara,afya na maji  ambapo wataalamu kutoka TARURA,RUWASA  na TANESCO walitoa majibu na ufafanuzi uliowapa wananchi hao matumaini mapya.

Kwa upande wao wanafunzi wa shule ya Sekondari Ghorowa iliopo kata ya Ayasanda, katika risala yao mbele ya Mbunge waliomba kuongezewa vitanda katika hosteli yao kwa kuwa wanalala kwa kubanana kutokana na upungufu uliopo.

Mheshimiwa Sillo katika kuhakikisha wananchi wanajibiwa kwa usahihi maswali yao,katika ziara yake kwenye Kata mbalimbali za Jimbo la Babati vijijini anaongozana na wataalamu wa Afya, Elimu,TARURA, RUWASA,Misitu na wengine hatua inayosaidia kuondoa malalamiko miongoni mwao.
Share To:

Post A Comment: