Na Munir Shemweta, WANMM MTWARA
Wakati Juni 23, 2021 ikiwa ni kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imepongezwa kwa uamuzi wake wa kuwatembelea watumishi wa sekta hiyo walioko ofisi za pembezoni kwa kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi changamoto za kitumishi .

Wakizungumza mkoani Mtwara jana, baadhi ya watumishi wa sekta hiyo walisema uamuzi uliofanywa kutuma maafisa kusikiliza changamoto za watumishi wa sekta hiyo katika ofisi za pembezoni siyo tu unasaidia kuwaondolea kero za kiutumishi bali unawapa faraja kuwa Wizara ya Ardhi iko pamoja nayo.

Walisema, mara kadhaa watumishi wanaofanya kazi maeneo ya pembezoni wanasahaulika katika masuala mbalimbali zikiwemo fursa za mikopo na hata vitendea kazi.

"Utaratibu uliofanywa na Wizara ya Ardhi kipindi hiki cha Wiki ya Utumishi wa Umma unatakiwa uwe endelevu kwa kuwa watumishi wanaofanya kazi pembezoni wanazo changamoto nyingi ukilinganisha na wanaofanya maeneo mengine" alisema Daniel Nguno Afisa Mipango Miji mkoa wa Mtwara.

Wizara ya Ardhi kwa mwaka huu imeamua kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma kwa kutembelea watumishi wake walioko ofisi za pembezoni ambazo ni zile zilizoko katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi.

Naye Mkuu wa Idara ya Ardhi halmashauri ya Nanyumbu Dikson Makombe alishukuru hatua ya Wizara kutembelea watumishi wa sekta hiyo ofisi za pembezoni kwa kusema  wao kama watumishi wamefarijika sana kwa kuwa hawajawahi kupata ugeni wa aina hiyo kwa kipindi kirefu na kusisitiza kupitia ujio huo wa Wizara wamejifunza mengi kuhusiana na masuala ya utumishi.

Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mtwara Rehema Mwinuka aliishukuru Wizara ya Ardhi kwa kuchagua mkoa wake kuwa miongoni mwa mikoa iliyotembelewa na timu ya Wizara hasa ikizingatiwa kuna jumla ya mikoa 26  na kueleza kuwa ni matumaini yake changamoto zilizowasilishwa na watumishi zitapata ufumbuzi.

Awali Afisa Utumishi wa Wizara ya Ardhi Bi. Mwajabu Masimba aliwataka watumishi wa sekta hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano huku  wakizingatia kanuni, taratibu na sheria za utumishi wa umma.

Alisema, uamuzi wa kutembelea ofisi za ardhi za pembezoni una lengo la kuonesha kuwa watumishi hao hawajatengwa sambamba na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili watumishi hao.

Halmashauri ambazo timu ya Wizara ilizungumza na watumishi wake katika mkoa wa Mtwara ni Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mtwara DC, Nanyamba Mji, Newala Mji, Newala DC, Masasi Mji, Masasi DC, Nanyumbu pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Tandahimba.

Wiki ya Utumishi wa Umma imeanza kuadhimishwa tarehe 16 Juni 2021 na imefikia kilele Juni 23, 2021 na kauli mbiu ya mwaka huu ni kujenga afrika tunayoitaka kupitia utamaduni wa uadilifu unaostawisha uongozi wenye maono hata katika mazingira ya mgogoro.
Share To:

Post A Comment: