Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo akizungumza wakati akifungua majadiliano yaliyohusu uhusiano baina ya maeneo maalum ya uwekezaji na uchumi wa ndani ambapo wadau mbalimbali wanaojihusisha na masuala ya uwekezaji wameshiriki.

 

Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Uwezeshaji wa Uwekezaji wa EPZA akitoa mada iliyohusu fursa zinatolewa na maeneo maalum ya uwekezaji na namna ambavyo Serikali za mitaa na biashara ndogo na za kati zinavyoweza kunufaika.

Mmoja ya wadau akiwa makini kusoma kijarida cha EPZA wakati wa majadiliano hayo yakiendelea.

Wadau wa uwekezaji, wafanyakazi wa Taasisi ya Uongozi pamoja na wafanyakazi wa EPZA wakifuatilia kwa makini hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo(hayupo pichani.)


Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo akiwa katika picha ya pamoja na wadau mara baada ya kufungua majadiliano yaliyohusu uhusiano baina ya maeneo maalum ya uwekezaji na uchumi wa ndani ambapo wadau mbalimbali wanaojihusisha na masuala ya uwekezaji wameshiriki

 …………………………………………………………..

Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo (MB) amewataka wadau wote hususan Taasisi za Serikali wanaohusika katika kuwezesha uwekezaji wa viwanda katika maeneo maalumu ya uwekezaji, kuhakikisha uwekezaji katika maeneo hayo unafanyika kwa ufanisi kama ilivyokusudiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa bila kufanya taratibu hizo kuwa kikwazo katika uwekezaji.

Prof. Kitila Mkumbo aliyasema hayo wakati akifungua kongamano la mahusiano kati ya maeneo maalumu ya uwekezaji na uchumi wa ndani lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi Tanzania (Uongozi Institute,) pamoja na Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) lililofanyika Juni 19, 2021 jijini Dar es salaam.

Akifungua Kongamano hilo, Prof. Mkumbo alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele katika uendelezaji wa Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (SEZ). Aidha Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 unasisitiza ustawishaji wa viwanda kwa maendeleo ya kiuchumi na watu kwa lengo la kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 (TDV 2025) inayolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi shindani na endelevu ifikapo mwaka 2025.

Aidha, Prof. Mkumbo alisema Wizara ya Viwanda na Biashara imejipanga kuendeleza viwanda vya kimkakati vinavyounganisha sekta mbalimbali, kuvutia na kuwezesha uanzishwaji na upanuzi wa viwanda vinavyotoa ajira kwa watu wengi, vinavyotumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini hususani kuongeza thamani katika mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu, na madini ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, kuongeza kipato, na  kuleta uwiano mzuri wa kiuchumi na kijamii mijini na vijijini.

Prof. Mkumbo pia alianinisha baadhi ya masuala muhimu ambayo mwekezaji huyazingatia kabla ya kuwekeza katika maeneo maalumu kuwa ni pamoja na Masoko ya uhakika ndani ya Tanzania na nje ya Nchi, Upatikanaji wa ardhi nzuri isiyokuwa na migogoro ya umiliki wala athari kwa mazingira, Uwepo wa miundombinu ya ndani (on-site infrastructure) kama barabara, maji, umeme na mawasiliano na uwepo wa nishati ya uhakika kwa maana ya umeme na gesi inayopatikana kwa bei ushindani,

Masuala muhimu mengine yaliyoainishwa ni pamoja na Upatikanaji wa rasilimali watu wenye ujuzi na stadi zinazoendana na shughuli wanazofanya viwandani na kwa gharama itakayoweza kuwapa ushindani,Miundombinu ya uchukuzi kuingiza malighafi viwandani na kutoa bidhaa zinazozalishwa kuelekea katika masoko mbalimbali na Vivutio vya uwekezaji vya kifedha (“fiscal incentives”) na visivyo vya kifedha (“non-fiscal incentives”) sambamba na utulivu wa nchi kisiasa na kiusalama.

Prof. Mkumbo alisema, katika kuhakikisha uchumi wa nchi unashindana kimataifa Serikali inaendelea kujiunga na jumuiya mbalimbali za kikanda na kimataifa kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ili kushindana kimataifa ili kuimarisha biashara ndani ya Afrika na nje ya mipaka kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kukuza uchumi wa taifa.

”Serikali imejipanga kisera na kisheria kutoa huduma muhimu katika maeneo ya uwekezaji, ujuzi muhimu katika elimu ili kwenda na matakwa ya soko kwa ujumla pamoja na sheria za kodi katika kuhakikisha uwepo wa uzalishaji wenye tija katika maeneo ya uwekezaji wa viwanda.” Alisema.

Aidha, Waziri aliiagiza EPZA kuongeza bidii ya kuelimisha umma kuhusu dhana ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji na kutangaza fursa na manufaa yanayotokana na uwekezaji huo pamoja na kujifunza kutokana na uzoefu wa nchi nyingine zinazofanya mageuzi ya kiuchumi nchini mwao kwa kujenga uchumi wa viwanda kupitia Maeneo Maalumu ya Uwekezaji, na kuleta uzoefu huo nchini kwa kuzingatia mazingira ya nchi yetu.

Serikali imejipanga katika ujenzi wa mitaa ya viwanda “Industrial parts” pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji katika maeneo ya uwekezaji ya Kurasini, Bagamoyo na Benjamin Mkapa mkoani Dar es Salaam ili kuhakikisha SEZ zilizopo zinatimiza malengo yaliyokusudiwa ya kukuza uchumi imara wa viwanda na kuimarisha ustawi wa wananchi ifikapo mwaka 2025. Alisema Prof. Mkumbo.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA,), John Mnali alisema Mamlaka hiyo imekuwa ikitekeleza majukumu katika maeneo ya uwekezaji kwa niaba ya Serikali kwa kuhakikisha maeneo yote ya uwekezaji yanapata huduma muhimu hasa miundombinu ya maji, umeme na barabara pamoja na kutoa leseni za uwekezaji kwa wawekezaji hao.

Kongamano hilo lilijumuisha wawakilishi wa Serikali za Mitaa, Viwanda vidogo na Biashara ndogo na kati, Kampuni za uwekezaji, Taasisi za Fedha, Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara walio kujadili fursa za uwekezaji wa viwanda kupitia Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (Special Economic Zones (SEZ)), kuainisha changamoto zinazohusiana na uwekezaji katika maeneo hayo na kuzitafutia ufumbuzi.

Aidha, Washiriki wa kongamano hilo walitembelea Benjamin William Mkapa Special Economic Zone ambayo ni eneo maalumu na mahususi kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa kwa mauzo ya nje ya nchi iliyojengwa na Serikali ya Awamu ya Tatu ili kuona mandhari yake, shughuli zinazofanyika na kujifunza kwa vitendo namna uwekezaji katika eneo hilo unavyochangia katika ukuaji uchumi wa ndani.


Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: