Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akizungumza wakati wa Semina ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu majukumu, muundo, mafanikio, changamoto na mikakati ya kutatua changamoto zinazoikabili Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) iliyofanyika bungeni jijini Dodoma. Wa pili kutoka kushoto ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai akifuatiwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua jambo wakati wa Semina ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu majukumu, muundo, mafanikio, changamoto na mikakati ya kutatua changamoto zinazoikabili Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) iliyofanyika bungeni jijini Dodoma

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt. Christine Ishengoma,akizungumza na wajumbe pamoja na washiriki wakati wa Semina ya Kamati hiyo kuhusu majukumu, muundo, mafanikio, changamoto na mikakati ya kutatua changamoto zinazoikabili Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) iliyofanyika bungeni jijini Dodoma

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Viongozi na Wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa kuhusu Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) wakati wa semina iliyofanyika bungeni jijini Dodoma.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Kunti Majala,akiuliza swali baada ya kumalizika kwa uwasilishaji wa taarifa kuhusu Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) wakati wa semina iliyofanyika bungeni jijini Dodoma.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa (CCM) Dkt.Bashiru Ally akichagia mada mara baada ya kumalizika kwa uwasilishaji wa taarifa kuhusu Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) wakati wa semina iliyofanyika bungeni jijini Dodoma.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM) Prof.Patrick Ndakidemi akichagia mada mara baada ya kumalizika kwa uwasilishaji wa taarifa kuhusu Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) wakati wa semina iliyofanyika bungeni jijini Dodoma.

........................................................................................

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imepewa semina kuhusu Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kwa malengo ya kujua majukumu yake, muundo wake, utekelezaji wa bajeti, mafanikio, changamoto na mikakati ya kutatua changamoto hizo.

Kamati imepatiwa semina hiyo bungeni jijini Dodoma katika ukumbi wa Msekwa D ambapo viongozi wa Wizara waliongozwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega.

Akizungumza kuhusu semina hiyo Mhe. Ulega amesema kuwa wizara imeona ni wakati muafaka kufanya semina kuhusu NARCO ili wajumbe wa kamati hiyo waweze kuielewa na kutoa maoni yao ambayo yatasaidia sana katika kuhakikisha kampuni hiyo inaendelea kuimarika kwa kuongeza uzalishaji wa mitamba, nyama na kuzidi kuchangia kwenye pato la taifa.

Mhe. Ulega amesema kuwa Kampuni hiyo ya Ranchi za Taifa ilipita katika kipindi kigumu na hivyo kushindwa kujiendesha lakini kutokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na wizara kwa sasa Kampuni hiyo inajiendesha yenyewe.

Katika taarifa iliyowasilishwa kwenye Kamati hiyo, imeainisha mafanikio yaliyopatikana, mipango iliyopo ya kuongeza uzalishaji na maeneo ya vipaumbele yaliyopo katika bajeti ya mwaka 2020/2021. Maeneo hayo ni Kuboresha Ranchi tano (5) za Kongwa, Ruvu, Kalambo, Missenyi na West Kilimanjaro ili kuongeza tija katika mnyororo wa thamani wa mazao ya Mifugo, Kuongeza uzalishaji wa ng’ombe kwa njia ya Uhimilishaji (AI) - kwa kutumia mbegu bora za ng’ombe wa nyama kama vile Boran na Simental.

Maeneo mengine ni Kudhibiti vifo vya mifugo kwa kiwango kisichozidi 2% ya wastani wa mifugo, Kuongeza na kuboresha nyanda za malisho kwa kudhibiti na kuondoa vichaka na kuimarisha vyanzo vya maji na Kuweka alama za kuonekana katika mipaka ya ranchi, kuondoa wavamizi na kuimarisha ulinzi wa mipaka.

Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Dkt. Christina Ishengoma amesema sasa ni wakati muafaka kwa Ranchi za Taifa kuanza kuzalisha malisho kwa ajili ya mifugo ambayo yataweza kuwasaidia hata wafugaji wanaozizunguka ranchi hizo. Vilevile ameshauri ranchi hizo ziweze kutumika kama mashamba darasa ambapo wafugaji hasa wa maeneo ya jirani wataweza kupata elimu juu ya ufugaji bora.

Akichangia baada ya taarifa kuwasilishwa mjumbe wa kamati hiyo, Mhe. Prof. Patrick Ndakidemi amesema kuwa ni wakati muafaka kwa kamati kuisaidia NARCO.

Prof. Ndakidemi amesema kwa kuwa tayari kampuni hiyo imeshaandaa andiko mradi, ni vema wajumbe hao wakalisoma hilo andiko na kuona ni maeneo yapi kamati inaweza kuisaidia kampuni hiyo. Vilevile amewasihi NARCO kuendelea kuyatunza na kuyalinda maeneo yao kwani yanawasaidia wafugaji wenye changamoto ya maeneo ya malisho kwa kuwakodishia.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: