Na Dismas Lyassa, Kibaha


WANANCHI wa Mtaa wa Mkombozi Kata Pangani katika Halmashauri ya Mji Kibaha wameomba Serikali kuongeza nguvu za kuwapatia huduma mbalimbali zikiwamo umeme, maji, zahanati na daraja ili kuharakisha maendeleo katika eneo lao.


“Tuna changamoto nyingi katika eneo letu, kwa mfano tangu kuumbwa kwa ulimwengu kuna barabara hadi leo hazijawahi kufunguliwa, tunapita kwenye majani na njia ni mbaya sana, magari huwa yanakwama hasa mvua zinaponyesha,” anasema mkazi mmoja wa mtaa huyo Ali Mohammed Juma.


Wakizungumza jana katika ziara ya Diwani wa Kata ya Pangani aliyoifanya Mtaa wa Mkombozi kuzungumza na mamia ya wananchi waliokosa umeme, wananchi mbalimbali walisema kuna idadi kubwa ya wananchi hawajapata umeme na wanaomba Serikali kuwasaidia kupata nishati hiyo muhimu.


“Tunaomba sana kusaidiwa tupate haraka umeme, lakini pia barabara zetu mbovu, hatuna zahanati wala kituo cha polisi. Serikali ya Mtaa inapambana kusaidia mambo kadhaa yakiwamo kushirikiana na wananchi kujenga shule na kadhalika, lakini tunaomba sana Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Halmashauri ya Kibaha kutusaidia kupata umeme kwa wananchi wote wenye uhitaji,” alisema Anuari Mweta, Mkazi wa Balozi namba tatu katika Mtaa huo wa Mkombozi.


Wakizungumza katika mkutani huo, wananchi walisema katika maeneo yote ya Mtaa wa Mkombozi wenye balozi sita, kila ubalozi kuna wananchi wanalalamikia kutokamilishiwa umeme. Aidha wananchi wanalalamikia kutokuwepo huduma za maji, hali inayosababisha wananchi kutumia vidimbwi ambavyo sio salama kwa matumizi ya wanadamu.


Kwa upande wake Diwani wa Kata Pangani, Agustino Mdachi aliwatia moyo wananchi kuwa na uvumilivu akidai kwamba huduma hizo zinafanyiwa kazi, zitapatikana. Kauli hiyo haikuwafurahisha wananchi wengi ambao walisisitiza na kuomba Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Kibaha kuangalia namna ya kuwatatulia changamoto mbalimbali zinazowasumbua ikiwamo kuwapatia maji hata kama kwa kuchimba visima vikubwa na kusambaza maji kwa wananchi wakati wakisubiri maji ya bomba ambayo haijulikani yatapatikana lini.


Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mkombozi, Anasi Bwanari alisema anaendelea na jitihada za ujenzi wa Shule ya Msingi Mkombozi na kuwaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano wa kukamilisha ujenzi huo huku wakisubiri fedha za kumalizia ujenzi kutoka ofisi ya Halmashauri.


“Ombi langu kwa wananchi wa Mtaa wa Mkombozi tuendelee kushirikiana kufanya kile ambacho kiko ndani ya uwezo wetu wakati tukisubiri nguvu kutoka katika ofisi nyingine za Serikali au wadau wengine wa maendeleo,” alisema Bwanari na kuahidi kushirikiana na wananchi na taasisi nyingine za Serikali ili kupata majibu kwa changamoto zilizoko katika Mtaa wa Mkombozi.


Eneo la Mkombozi tayari limefikiwa na Mradi wa Umeme Vijijini (REA) lakini kuna wananchi hawajapatiwa nishati hiyo, huku hawajui ni lini watapata huduma hiyo, kwa maelezo kuwa wanaahidia bila kuambiwa watapata lini hasa.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: