Katibu Mkuu wa TAMUFO, Stella Joel.

Mlezi wa TAMUFO, Frank Richard.


 Na Dotto Mwaibale

UMOJA wa Wanamuziki Tanzania ( TAMUFO) umempongeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa kwa kusikia kilio chao kwa kuwatoa hofu Wasanii kuhusu suala la ugawaji wa Mirabaha. 

Hatua hiyo ya Bashungwa imekuja ikiwa ni siku moja tu baada ya TAMUFO kuliomba  Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA)  kuhakikisha linashirikisha wadau wa muziki  kabla ya kutoa maamuzi ya kuwabana wasanii.

Ombi hilo lilitolewa na Katibu Mkuu wa TAMUFO, Stella Joel  jijini Arusha juzi baada  ya kutokea malalamiko ya wanamuziki kulalamikia kitendo cha Basata kuweka  utaratibu wa kuwataka wanamuziki nyimbo zao zikaguliwe baada ya kurekodi kwa  sababu za kimaadili.

Joel alisema jambo hilo lilikuwa linawaumiza wanamuziki wa Tanzania ambao wanahangaika sana kuwezakumudu gharama za kurekodi kazi zao.

Katibu mkuu huyo wa TAMUFO Stella Joel alisema wanamuziki wengi hawana kipato  cha kutosha na kurudia rudia katika kurekodi kazi zao na bado hawajaweza kufaidika nazo.

Akizungumza jana jijini Dodoma katika kikao chake na  Viongozi wa Vyama na Mashirikisho ya Muziki na Filamu nchini kilicholenga kuzungumzia Kanuni ya 26 ya BASATA inayohusu uhakiki wa kazi za Muziki na Filamu  kabla ya kuingia sokoni au kusambazwa, Bashungwa aliwatoa hofu wasanii kuhusu suala la ugawaji wa Mirabaha kwa kuelezea kuwa Serikali imeandaa mifumo ya kidijitali ambayo itarahisisha  ukusanyaji wa mirabaha hiyo na kuongeza gawio.

“COSOTA imekuwa na changamoto ya ukusanyaji wa mirabaha kutokana na uhaba  wa watumishi hivyo kwa kupitia mfumo mpya wa kidijitali utakao anzishwa hivi karibuni utarahisisha ukusanyaji wa mirabaha hiyo, Serikali inataka kutoa gawio la pesa nyingi kwa wasanii na siyo fedha kidogo hivyo tunawaomba mvumilie kidogo kuanzia mwaka mpya wa fedha mambo yatakuwa mazuri.” alisema Bashungwa.

Akiendelea kuzungumza katika kikao hicho Bashungwa alitoa maelezo mahususi kwa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) akiwataka kusitisha utekelezaji wa Kanuni ya 26 inayotaka kazi zote za Muziki kukaguliwa nao kabla ya kusambazwa.

Aidha, Bashungwa alisisitiza kuwa maelekezo hayo ya kusikitishwa kwa matumizi ya kanuni hiyo ni kwa upande wa Muziki pekee ila kwa upande wa Filamu itaendelea kutumika kama kawaida. 

Pamoja na hayo Bashungwa alitoa maelekezo ya haraka kwa BASATA kwa kuwataka kuanzisha mchakato wa kurekebisha kanuni hiyo kwa kuwashirikisha wadau  hao wa vyama na mashirikisho ili kuweza kupata Kanuni mpya isiyodumaza tasnia ya Muziki lakini izingatie maadili ya Taifa.

Halikadhalika Waziri huyo ameelekeza BASATA kwa kushirikiana na wadau kuandaa mwongozo utakao kuwa kukitoa dira njema ya uendeshaji na ukuzaji wa tasnia ya Muziki.  

Naye mmoja wa wasanii hao Soggy Doggy alimshukuru Bashungwa kwa maamuzi  aliyoyafanya na kumpongeza na kuahidi kuendelea kushirikiana na wasanii wa Muziki katika  kukuza na kuiendeleza tasnia ya muziki nchini.

Mlezi wa TAMUFO, Frank Richard, akiongea juzi na waandishi wa habari  aliiomba Serikali kuziwezesha taasisi zenye nia ya kusaidia maendeleo ya sanaa hapa nchini Ikiwemo Basata.

Richard aliomba kuwepo na 
 utaratibu wa kuandaa semina kwa ajili ya kutoa elimu ya kuwajengea uelewa wasanii juu ya kazi zinazokubalika kimaadili na katika kulinda heshima ya muziki na utamaduni wa Tanzania.

Aidha Richard ameoimba Serikali kuhakikisha idadi ya studio zote hapa nchini zinajulikana ili kuweza kutoa elimu kupitia vipeperushi vinavyozungumzia maadali na taratibu zinapaswa kufuatwa kabla ya kutoa wimbo.

Alisema hali hiyo itaepusha hasara zinazosabisha msanii kurudia wimbo pia kuepusha malalamiko hayo yanayojitokeza.

Richard alisema taasisi zinazosimamia kazi za sanaa na wasanii kwa Ujumla ni muhimu ziandae vipindi vya Redio na Tv na mitandao ya Kijamii kwa ajilo ya kutoa elimu kwa wasanii na wamiliki wa studio  ili kuwajengea uelewa   juu ya jambo hilo.


Share To:

Post A Comment: