Na James Mhilu - Arusha


Serikali imesema kuwa hakuna upungufu wa chanjo kwa akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano na kwamba chanjo hizo zipo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na hospitali na kwamba zinatolewa bure bila malipo .


Akizungumza na wataalam wa afya katika Kituo cha Afya Kaloleni Halmashauri ya Jiji la Arusha  Mkurugenzi wa Kinga  kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi amesema taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu upungufu wa chanjo hazina uhalisia na kwamba chanjo iko ya kutosha katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya nchini .


Dr. Subi alisema kuwa ni jukumu la wataalam wa Afya kuwahudumia wanawake na watoto bila kikwazo ikiwa ni njia mojawapo yakupunguza na kuondoa kabisa vifo vya akina mama na watoto nchini .


Aliongeza kuwa kuwa Serikali ya awamu ya sita inawajali wanawake na watoto nakuwa wataalam wa Afya wanajukumu lakuhakikisha kuwa kundi hilo linapata huduma bora bila kikwazo .


Pia aliagiza Waganga wakuu wote nchini kuhakikisha wanaweka Televisheni na vipeperushi katika vituo vya kutolea huduma za Afya hususani katika majengo wanayohudumia akina mama wajazito na kuweka vipindi vinavyoelimisha akina  mama juu  ya afua mbali mbali za Afya ya uzazi na jinsi ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyo ya kuambukiza.


“Naagiza Waganga wakuu wote nchini kununua na kuweka Televisheni katika vituo vya kutolea huduma za Afya na hospitali ili kuwapatia fursa akina mama kujifunza afya ya uzazi ikiwa ni njia ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito .” alisema  Dkt. Subi.


Pamoja na mambo mengine aliwataka akina mama wajawazito kujali Afya zao kwa kuhudhuria Kliniki kwa wakati ili kupata huduma bora ikiwa ni pamoja na kulinda watoto waliopo tumboni .


“Niwaombe akina mama mjali Afya zenu pamoja na kulinda haki zenu kwa kuhakikisha kuwa hakuna mtaalam anayekuonea pindi unapofika hospitalini au vituo vya afya kwa kuwa ni haki yenu kupata huduma ya afya bila kikwazo 

“ anasema Dk. Subi 


Hata hivyo alipongeza Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa huduma bora za afya kwa wananchi ikiwemo akina mama na watoto kuwa utamaduni huo unapaswa kuendelezwa ikiwa ni kuendelea kuwahimiza wanaume kusindikiza wake zao katika vituo vya afya na hosiptali .


Dr.subi alisema wanaume wanamchango mkubwa katika kuhakikisha wake zao wanajifungua salama ikiwa ni kuhakikisha kuwa wamehudhuria katika kliniki kwa wakati .


Mganga mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dkt. Kheri Kagya alisema kuwa maagizo ya Serikali yatafanyiwa kazi na kwamba Halmashauri ya Jiji la Arusha ina chanjo yakutosha na kwamba walengwa wanapata bila kikwazo .

Share To:

msumbanews

Post A Comment: