Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi mara baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa Ulemo-Misigiri Machi 16, 2021.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) Mhandisi Patrick Nzamba akiwasilisha taarifa ya mradi wa maji Misigiri kwa Mkuu wa wilaya ya Iramba wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa Ulemo-Misigiri.
B
baadhi ya wananchi wa Misigiri wakifuatilia tukio la uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa maji wa Ulemo-Misigiri

 

 

Na Mohamed Saif

Serikali imewasisitiza wananchi kuhakikisha wanatunza miradi ya maji inayojengwa kwenye maeneo yao ili iweze kutumika na vizazi vijavyo.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa Ulemo Misigiri Machi 16, 2021.

Luhahula alisisitiza kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miradi ya maji na hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha miradi inakuwa endelevu kwa matumizi ya sasa na ya vizazi vijavyo.

“Wananchi hakikisheni mnatunza na kulinda miundombinu ya mradi huu, tunatambua changamoto hapa ni maji na bahati nzuri Serikali imewaletea mradi itashangaza kuona mnautelekeza,” alisisitiza Mkuu wa Wilaya Luhahula.

Aidha, aliwasisitiza wataalam wanaotekeleza mradi huo kuhakikisha suala la thamani ya fedha linazingatiwa ili mradi unaojengwa uwe katika ubora unaokubalika.

“TAKUKURU wapo macho wanaangalia fedha inayotumika hapa ipo sawa na mradi ama shughuli inayofanyika kwenye mradi sasa hili mlizingatie mradi ujengwe kwa ubora wake,” alisema Luhahula.

Aliwataka wananchi kuhakikisha mradi unapoanza kazi wautumie ipasavyo kuwaletea maendeleo hasa ikizingatiwa kwamba maji yatakayotokana na mradi huo ni safi na salama na kwamba waepuke kutumia maji ambayo sio safi na salama.

Akiwasilisha taarifa ya mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) Mhandisi Patrick Nzamba alisema mradi unatekelezwa na wataalam wa ndani kwa gharama ya shilingi milioni 569.

Alisema utakamilika Juni, 2021 na kwamba utanufaisha zaidi ya wananchi 9000 kutoka Kata za Ulemo na Misigiri “Mradi huu utakapokamilika utatutoa kwenye asilimia 57 za sasa za upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama na maeneo haya yatakuwa na upatikanaji wa majisafi kwa asilimia 100,” alisema Mhandisi Nzamba.

Hafla hiyo ya uwekaji wa jiwe la msingi wa mradi wa Ulemo-Misigiri unakwenda sambamba na uzinduzi wa miradi na uwekaji wa jiwe la msingi maeneo mbalimbali kote nchini ikiwa ni kuadhimisha Wiki ya Maji mwaka 2021 inayoanza leo Machi, 16 hadi Machi 22, 2021.

 

Share To:

Post A Comment: